Dante, Yanga ngoma bado mbichi kabisa

Muktasari:

  • Uongozi wa Yanga, Mwanasheria wa mchezaji huyo, Alfred Mtawa pamoja na Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji walikutana Oktoba 18 kutatua suala lao, lakini kwa upande wa Yanga uliomba siku 18 ili umalizane nao.

SAKATA la beki Andrew Vincent ‘Dante’ na uongozi wa Yanga limezidi kushika kasi baada ya vuta ni kuvute inayoendelea kati ya pande mbili.
Iko hivi, Dante alijiondoa katika kikosi cha Yanga msimu huu baada ya kudai malimbikizo ya pesa zake za usajili na sehemu ya mishahara yake.
Uongozi wa Yanga, Mwanasheria wa mchezaji huyo, Alfred Mtawa pamoja na Kamati ya Sheria na Hadhi ya wachezaji walikutana Oktoba 18 kutatua suala lao, lakini kwa upande wa Yanga uliomba siku 18 ili umalizane nao.
Mwanaspoti liliripoti awali kwamba, pande hizo mbili zilikutana, lakini zilishindwa kumalizana na Novemba 2 zilirejea kwenye kamati hiyo ambapo uongozi wa Yanga uliomba tena siku saba za kukaa na kupitia upya shauri hilo kutokana na mabadiliko ya kiofisi yaliyofanyika.
Hata baada ya kupewa siku hizo, Mwanaspoti lilipenyezewa kwamba hakuna nguvu iliyotumika kwa Yanga kumtafuta mwanasheria huyo wala mchezaji husika ili kupatana kama ambavyo kamati iliwaelekeza.
Mwanaspoti lilimtafuta mwanasheria wa Dante, Mtawa aliyesema uongozi wa Yanga umekaa kimya licha ya kuomba siku hizo, hivyo suala hilo wanaliacha kwa kamati ya TFF kufanya uamuzi.
“Walipewa siku saba ambazo zilikuwa zinaisha Jumatatu, huwezi amini ni kwamba hakuna chochote kilichofanyika mpaka hivi sasa, tumerejesha majibu TFF ya kimaandishi kama ambavyo walituelekeza,” alisema.
Alisema tayari wameshapeleka barua ya majibu TFF, baada ya kuona uongozi wa Yanga unawapotezea kumaliza tatizo hilo.
Alipoulizwa juu ya suala la mchezaji huyo kutomalizika hadi sasa, ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema anachofahamu ni kwamba jambo hilo litamalizwa na kuwa, mchezaji huyo atalipwa kidogo kidogo iwe ni kupitia TFF au timu yenyewe kumlipa.