Dau la Msuva kikwazo kwake kuondoka Morocco

Muktasari:

Msuva (24), amedai kwamba mmiliki wa klabu hiyo amepanga kumuuza kwa dau la Dola 2 milioni kwa klabu mbalimbali za Bara la Ulaya ambazo zimekuwa zikiiwania saini yake na klabu hizo zimekuwa zikikimbia pindi zikitajiwa dau hilo

STAA wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Simon Msuva amesema dau kubwa ambalo mmiliki wa klabu yake ya Difaa Jadida amepanga kumuuza ndio kikwazo kikubwa kinachoendelea kumbakisha katika soka la Morocco mpaka sasa.
Msuva (24), amedai kwamba mmiliki wa klabu hiyo amepanga kumuuza kwa dau la Dola 2 milioni kwa klabu mbalimbali za Bara la Ulaya ambazo zimekuwa zikiiwania saini yake na klabu hizo zimekuwa zikikimbia pindi zikitajiwa dau hilo.
“Mmiliki wetu anaamini mimi nina thamani kubwa. Huwa anazitajia klabu dau la Dola 2 milioni sasa brother klabu zinahoji iweje niuzwe thamani hiyo wakati timu yetu haishiriki hata michuano ya Afrika. Hii imekuwa tatizo,” alisema Msuva katika mahojiano ya Mwanaspoti hapaTunisia.
“Kilichobakia kwa sasa naendelea kujituma zaidi na kuisaidia klabu yake lakini hilo dau ni kubwa. Nadhani mwenyewe ameridhika niendelee tu kuipatia timu mafanikio lakini kama ni kuuzwa inabidi hilo dau lishuke,” alisema Msuva.
Msuva pia amedai kwamba beki wa kushoto wa Tanzania anayekipa naye El Jadida, Nickson Kibabaige ataibuka kuwa kati ya mmoja wa mabeki bora wa pembeni katika soka la Morocco na amekuwa akiulizia maendeleo yake ndani kwa ndani kwa kocha wetu mpya, Badou Zakhi.
“Kibabage ninaishi naye nyumbani. Nimekuwa nikiulizia maendeleo yake kwa Kocha Zakhi na amenihakikishia atakuwa tishio siku za usoni. Unajua alikuja huku kwa ajili ya timu ya vijana, lakini amekuwa akifanya mazoezi nasi na amekuwa akipangwa katika baadhi ya mechi za timu za wakubwa,” alisema Msuva.