De Gea aumia Manchester United ikijianda kuivaa Liverpool

London, England. Hofu imetanda Manchester United kujua hatma ya hali ya majeruhi ya kipa wao David de Gea aliyeumia wakati akichezea Hispania jana usiku dhidi ya Sweden.

Kipa De Gea alilazimika kutolewa baada ya kuumia misuli wakati wa mchezo huo wa kusaka kufuzu kwa Euro 2020 dhidi ya Sweden.

De Gea alionekana ameumia baada ya kuokoa pasi aliyopewa katika dakika 60, na kulazimika kutolewa nafasi yake kuchukuliwa na kipa wa Chelsea, Kepa Arrizabalaga.

Kocha Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer anatumaini majeruhi hayo si makubwa wakati huu akijianda kwa mchezo dhidi ya Liverpool utakaopigwa Old Trafford Jumapili ijayo.

Kocha wa Hispania, Robert Moreno alisema kuhusu hali ya De Gea: 'Amepata maumivu ya misuli ya nyonga, lakini alipewa matibabu wakati wa mapumziko na alitaka kuendelea kucheza. Alituhakikishia, lakini alishindwa kuendelea na mchezo.'

Katika muda wa nyongeza mshambuliaji aliyeingia akitokea benchi Rodrigo Moreno alifunga bao la kusawazisha kwa Hispania baada ya Sweden kufunga bao la mapema kupitia Marcus Berg katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.