De Ligt afuata ushauri wa Ronaldo, atua Juventus

Muktasari:

  • Beki huyo Mholanzi alishauriwa na Ronaldo kujiunga na vigogo hao wa Turin wakati wawili hao walipokutana katika fainali ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya iliyopisha kwa Ureno kutwaa ubingwa.

Rome, Italia. Beki Mholanzi wa kati, Matthijs de Ligt leo amesaini mkataba wa kuichezea Juventus kwa ada ya dola 84.2 milioni za Kimarekani, akitokea Ajax, mabingwa hao wa soka wa Italia wametangaza.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 19 amesaini mkataba wa miaka mitano.
Juventus ilisema katika taarifa yake kuwa fedha hizo zitalipwa katika kipindi cha miaka mitano ya fedha, pamoja na "gharama za ziada" ambazo ni euro 10.5 milioni.
Ada ya De Ligt inamfanya kuwa mchezaji ghali anayeshika nafasi ya tatu katika klabu ya Juventus akiwa nyuma ya Ronaldo (euro milioni 105 mwaka 2018) na Gonzalo Higuin (euro 90 milioni mwaka 2016).
De Ligt pia alikuwa akihusishwa na mipango ya kuhamia Manchester United, Barcelona na Paris Saint-Germain baada ya kuonyesha kiwango kikubwa ambacho kiliiwezesha Ajax kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu uliopita.
Mchezaji mwenzake wa Ajax mwenye umri wa miaka 22, kiungo Frenkie de Jong, ameshajiunga na Barcelona.
De Ligt alicheza mechi 117 akiwa na na Ajax katika mashindano tofauti na kufunga mabao 13 na ndiye aliyefunga bao la ushindi mjini Turin wakati Ajax ilipoiondoa Juventus katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
De Ligt ameshaichezea timu ya taifa ya Uholanzi mara 17, akiunda beki pacha ngumu pamoja na Virgil van Dijk wa Liverpool.
Aliteuliwa kuwa nahodha wa Ajax Machi 2018 na hivyo kuwa nahodha mwenye umri mdogo kuwahi kutokea katika klabu hiyo.
De Ligt alisema Ronaldo alimshauri ajiunge na Juventus baada ya wawili hao kukutana katika fainali ya Ligi y Mataifa ya Ulaya mwezxi Juni na Ureno kuibuka bingwa.