Diamond? Mbona mambo freshi tu

Thursday January 31 2019

 

By Rhobi Chacha

Kama unakumbuka msanii wa Bongo Fleva, Rich Mavoko aliwahi kufikisha malalamiko yake serikalini kwa kutoridhishwa na mkataba aliopewa na uongozi wake wa zamani, WCB, huku akidai sababu kubwa ni unyonyaji unaofanya na kampuni hiyo katika kufanya kazi na malipo kwa wasanii wao.

Hata hivyo, sakata hilo lilimalizika na Mavoko kushinda kesi dhidi ya Label yake hiyo ya zamani WCB na kufanikiwa kuvunja mkataba na kutoka. Hivyo kwa sasa jua hakuna bifu katika ya pande hizo mbili.

Mavoko ameliambia Mwanaspoti, kuondoka kwake WCB haimaanishi ana bifu na wahusika wowote wa kampuni hiyo, iwe wanamuziki ua hata viongozi wao kwani walimalizana kwa usalama.

“Kiukweli mimi sina tatizo na WCB, yaani hakuna bifu kati yetu na hili swali nimeshaulizwa sana na watu wa media na narudia tena mimi sina bifu na watu wa WBC na sikuondoka kwa ugomvi pale, ni mambo tu ya kawaida ya kimuziki.

“Hivi ninavyokwambia hata ikitokea kuna kazi inatakiwa kufanya pamoja, basi nipo tayari kukaa nao chini na kufanya nao kwani cha msingi tunaangalia biashara kama inalipa,” alisema Mavoko.

Mavoko ambaye amewahi kutamba na baadhi ya vibao kama Pacha Wangu, Marry Me, Rudi, Sheri anasema tangu ajiondoe WCB na kutoa nyimbo zake kama Navumilia, Hongera, Naogopa uelekeo wake wa muziki umezidi kushamiri na wala haujarudi nyuma kama baadhi ya mashabiki wanavyodai amepoteza uelekeo baada ya kuondoka WCB.

“Nashukuru Mungu tangu nimejiondoa WCB na kufanya kazi kivyangu kama zamani, maendeleo ya muziki kwangu nayaona kutokana na mauzo ya kazi zangu.

“Na ukiona tu msanii anatoa wimbo siku moja na siku ya pili watu wanauimba, basi jua wimbo huo umepata mapokezi mazuri na hii imenikuta mimi katika nyimbo zangu zote ninazotoa, mashabiki zangu huwa wepesi kuimba na kujirekodi na kuposti katika mitandao.”

Aidha Mavoko alijibu swali aliloulizwa na Mwanaspoti kuhusu, kujutia kupoteza mashabiki baada ya kuondoka WCB kwani kampuni hiyo ina mashabiki wengi katika wanamuziki wao.

“Aise sijutii wala sidhani nimepoteza mashabiki wangu baada ya kujiondoa WCB, sababu mimi nawafahamu vizuri mashabiki zangu na wao wananifahamu mimi vizuri, hivyo huwa hawabadili na kuyumbishwa kwa kile wanachoamini watu wengine.

“Nasema hivi kwa sababu, mimi kama mimi Richard Martin mashabiki zangu ni wale wale ambao nimeanza muziki hadi kufikia hapa nipo nao, sambamba na wakati mwingine hao hao ndio wanakuwa washauri wangu, sasa mtu atakujaje kusema nimewapoteza? Hakuna kitu kama hicho.”

Mavoko alisema pia, ndio maana hata alipojiunga WCB mashabiki zake wapo waliofurahia na wengine kuchukizwa na kumwambia anaenda kupotea, lakini alijaribu kuwaelewesha na wakaelewa na kuwa nae pamoja.

Hata hivyo, Mavoko anasema kwa sasa yupo mtu anayemsimamia kazi zake, japo mtu huyo hayuko tayari kuanikwa hadharani.

“Unajua huu muziki wetu, hata kama unaujua kiasi gani, bila ya kuwa na mtu anayekusimamia utauona ni mgumu sana kutokana na uhitaji wa soko pana, hivyo ninao watu ambao hawataki waanikwe hadharani wao wanatenda kazi tu.”

Ishu ya penzi na Lulu Diva

Habari ambazo zinadaiwa zipo wazi katika mitandao ya kijamii na hata huko mitaani, Mavoko na msanii wa kike wa Bongo Fleva, Lulu Diva ni wapenzi, kitu ambacho Mwanaspoti liliwahi kuzungumza na Lulu Diva ishu hiyo na kukanusha na leo Mavoko anazungumzia hapa:

“Hizo ni habari kama habari zingine tu na mimi sijawahi kutamka au kukubali hadharani nina uhusiano wa kimapenzi na Lulu Diva, ila nikwambie tu hakuna kitu kama hicho, yale uliyokuwa unayasikia yalikuwa ni mambo ya kazi tu na kazi ilionekana kwenye wimbo ‘Ona’ wa Lulu Diva.

Hata hivyo, Mavoko anasema baada ya miaka mitano ijayo ana ndoto za kuwa mfanyabiashara mkubwa wa muziki.

“Kama unavyojua kila msanii huwa ana ndoto zake kichwani mwake, hivyo mimi ndoto yangu ni kuwa mfanyabiashara mkubwa wa muziki.

“Hata hivyo, hadi sasa nashukuru baadhi ya malengo yangu niliyojipangia katika muziki, yametia kwa asilia kadhaa, hivyo naimani hata hii ndoto yangu niliyokuwa nayo hapo baadae kuwa mfanyabiashara mkubwa wa muziki nitafanikiwa tu,” anasema Rich Mavoko.

Hata hivyo, Rich Mavoko ambaye ni msiri sana wa mambo yake binafsi kuyaweka hadharani kama baadhi ya wasanii wengi, amesema hakuna kitu kingine nachofanya nje ya muziki kwa sababu muziki ndiyo maisha yake na ndiyo kila kitu kwakwe.

Advertisement