Dili la kiungo Bruno Fernandes Manchester United limeyeyuka

DILI la kiungo wa Sporting Lisbon, Bruno Fernandes kutua Manchester United limeyeyuka rasmi baada ya timu hizo mbili kutofautiana katika suala la bei ya staa huyo wa kimataifa wa Ureno.

Inaelezwa kuwa Sporting Lisbon inataka Pauni 68 milioni iliyopo kwenye mkataba wa Fernandes ili kumuachia atue Old Trafford, lakini Man United imegoma kutoa dau hilo ikidai ni kubwa sana kulinganisha na thamani halisi ya kiungo huyo.

Badala yake Man United imeweka mezani Pauni 42.5 milioni, huku Pauni 8.5 milioni zaidi ikitarajiwa kuongezwa kutokana na kiwango na idadi ya mechi ambazo Fernandes atacheza pale Man United.

Licha ya Sporting kuwa tayari kumuuza Fernandes na Man United kumuhitaji sana kiungo huyo, lakini tofauti katika masuala ya pesa inaonekana kuua dili hilo ambalo lilitarajiwa kukamilika kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili la Januari. Hii itakuwa ni mara ya pili kwa kiungo huyo kukwama kutua Man United.