Dk Mwakyembe ajibu tuhuma za wasanii kumiliki madanguro

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe akijibu baadhi ya hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Tuhuma za wasanii nchini Tanzania kumiliki madanguro na kula fedha za misiba zilitolewa bungeni na mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku Musukuma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo mwaka 2019/2020

Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amesema hoja ya mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku Musukuma kuwa wasanii nchini wanamiliki madanguro na kula fedha za misiba, si ya kweli.

Dk Mwakyembe ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 23, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo.

Alhamisi iliyopita Aprili 18, 2019 Naibu Spika, Dk Tulia Ackson aliitaka Serikali leo kujibu madai ya wasanii wa filamu nchini kumiliki madanguro sambamba na kuchangisha fedha katika misiba na kuzitumia katika mambo mengine.

Suala la wasanii kumiliki madanguro na kutafuna fedha za misiba liliibuliwa na Musukuma katika mjadala huo na kumfanya Dk Tulia kutaka maelezo ya Serikali kwa kuwa kauli hiyo ikiachwa hivyo inaweza kuleta picha mbaya kwa wasanii.

Katika majibu yake Dk Mwakyembe amesema, “vitendo hivyo havikubaliki kisheria na ni kosa la jinai, nimuombe tu Waziri wa Mambo ya Ndani asilichukulie kwa nguvu suala hili (la madanguro na fedha za misiba) maana Musukuma alizungumza pengine kutaka kusikika tu.”

Katika maelezo yake ya Alhamisi iliyopita Dk Tulia alisema, “Kuna mchango ulitoka hapa naamini utakapopewa fursa ya kuhitimisha hoja yako utaliweka vizuri zaidi. Umekuja mchango kuhusu wasanii kuwa ndio wamiliki wa madanguro mengi Dar es Salaam.”

 “Nadhani  hili uliweke sawa halitakuwa jambo jema kama halina ukweli wowote kuwadhalilisha wasanii wetu.”

Kuhusu fedha za misiba, naibu Spika alisema, “pia kuna hoja ya ushiriki wa wasanii kwenye misiba kwamba wanakusanya michango na wanaweza kuitumia si kwa makusudi ya kukusanywa kwake. Haya mambo mawili yanawaweka wasanii wetu katika mazingira ambayo si mazuri.”

Siku hiyo kwenye mjadala Musukuma alianza kwa kueleza jinsi wasanii wa filamu nchini walivyo na hali mbaya kiuchumi, huku akihoji sababu za tamthilia za nje kutafsiriwa kwa Kiswahili na kuonyeshwa katika televisheni mbalimbali nchini, kwamba ndio kumechangia kuua tasnia ya filamu.

“Wasanii wa filamu hawana kitu sasa hivi wanategemea misiba wapate michango na kufungua madanguro na kuwa makuwadi kwa wanaume,” amesema Musukuma.