Failuna: Ndoto yangu ni medali ya dunia

Muktasari:

  • Wanariadha wengine watakaoiwakilisha nchi ni Alphonce Simbu, Agostino Sulle na Stephano Huche wataondoka nchini Oktoba 2 na watakimbia Oktoba 6 katika hafla ya kufungwa kwa mashindano hayo.

Dar es Salaam. Mwanariadha nyota wa timu ya Taifa, Failuna Abdi anatarajiwa kuondoka nchini kesho Jumanne kuelekea Qatar katika mashindano ya dunia.

Mwanariadha huyo amesema anakwenda katika mashindano hayo akiwa na ndoto ya medali ya dunia.

Failuna mwanariadha pekee wa kike aliyefuzu kuiwakilisha nchi katika mashindano hayo ataondoka nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia) kuelekea Doha, yanapofanyika mashindano hayo.

"Najua ugumu wa mashindano ya dunia, natarajia ushindani wa hali ya juu, lakini nimejiandaa na ndoto yangu ni kushinda medali," alisisitiza Failuna ambaye atachuana katika marathoni.

Failuna atapeperusha bendera ya Tanzania Ijumaa hii katika ufunguzi wa mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).