Felaini kufungiwa na FA

Muktasari:

Kiungo wa kimataifa wa Ubelgiji, Marouane Fellaini wa Manchester United dakika yoyote ataadhibiwa na Chama cha soka England (FA) kwa kufungiwa mechi tatu na kutozwa faini kutokana na kitendo chake cha kumvuta nywele kiungo chipukizi wa Arsenal, Matteo Guendouzi timu hizo zilipokutana jana.

London, England. Kiungo mahiri wa Ubelgiji, Marouane Fellaini yupo hatarini kufungiwa na Chama cha soka England (FA) kutokana na kitendo kisicho cha kiungwana cha kumvuta nywele Matteo Guendouzi.

Kiungo huyo wa Manchester United, alifanya kitendo hicho juzi katika mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa kwenye dimba la Old Trafford, iliyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mchezaji huyo ambaye mwezi uliopita alikuja na muonekano mpya baada ya kuzikata nywele zake ndefu alizozoea kuziacha katika mtindo wa Afro, alimvuta nywele chipukizi huyo wa Arsenal katikati ya Uwanja.

Mchezaji huyo ambaye tayari ana kadi sita ya njano msimu huu, alikuwa na bahati kwamba hakuonwa na mwamuzi kwa kitendo hicho, lakini ataingia matatani pale FA itakapopitia marudio ya mchezo huo.

Fellaini mwenye miaka 31 hakuonekana kujutia kitendo chake kwani alipohojiwa sababu za kufanya vile alijibu ikiwa yeye ameshindwa kuendelea kuwa na nywele ndefu ni mchezaji gani atakayeweza.

Mashabi wa soka kuanzia wale wa Arsenal hadi wa Man United wameitaka FA, kumchukulia hatua mchezaji huyo kwa kile alichomfanyia Guendouzi chipukizi mwenye mkiaka 19.

Kiungo huyo anakumbuka vizuri kilichompata beki wa kimataifa wa Ujerumani anayekipiga Leicester City, Robert Huth, alipomvuta Fellaini nywele mwaka 2016 ambapo FA ilimfungia michezo mitatu.

Mwamuzi wa mchezo huo, Andre Marriner amekiri kuwa hakuliona tukio hilo ndiyo sababu hakumpa Fellaini kadi, hivyo rungu linabaki kwa FA kumuadhibu.