Fifa yatenga Sh4 bilioni ujenzi kituo cha michezo Tanga

Wednesday May 8 2019

 

By Burhani Yakub

Tanga. Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe leo Jumatano ametembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha michezo na kuahidi kulihimiza Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuanza haraka mchakato wa kufanikisha.

Akizungumza katika eneo la Mnyanjani jijini Tanga lililotengwa kwa ajili ya kuendesha mradi unaofadhiliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wa kujenga kituo cha michezo, amesema kuna haja kwa TFF kuanza mara moja ujenzi wa kituo hicho.

"Gharama ya ujenzi wa kituo hicho ni zaidi ya Sh4 bilioni tayari FIFA imezitenga... "alisema Mwakyembe.

Mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF, Khalid Abdallah alimweleza Waziri kwamba kwa mujibu wa ramani ni kuwa vitajengwa viwanja vitatu ndani ya uwanja huo, kituo cha kufundishia soka kwa vijana na majengo mbalimbali yanahusiana na masuala ya soka.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Daudi Mayeji alisema eneo hilo lina ukubwa wa hekta 7.6 na kwamba tayari fidia imeshatolewa kwa nyumba zilizo ndani ya kituo hicho.

Waziri Mwakyembe pia alikagua uwanja wa Mkwakwani jijini hapa kuangalia hali ilivyo ya uwanja wa soka ambapo alisema kuna haja ya kuufanyia ukarabati ili wachezaji wasiumie

Advertisement

Advertisement