Francis Cheka Sikuhamia Msumbiji kwa bahati mbaya

Kupanga ni kuchagua. Ndivyo amefanya bondia bingwa wa zamani wa dunia wa WBF, Francis Cheka ‘SMG’.

Cheka, baba wa watoto watatu Boniface, Historia na Azenga anaishi nchini Msumbiji tangu Desemba 2018.

Nchini humo, Cheka anaishi Mueda na watoto wake wawili huku mmoja akisalia mjini Morogoro kwa mkewe, ambako amejenga nyumba mbili.

Tayari Cheka amewekeza nchini Msumbiji alikozaliwa mama yake, Maria Rafael, ambako amejenga nyumba na kuendeleza biashara yake ya chupa za plastiki ambayo amewahi kuifanya Morogoro na Mtwara kabla ya kuhamia huko.

“Nilifuata fursa Msumbiji, sikuja kwa bahati mbaya,” anaanza kusimulia Cheka ambaye kwa mashabiki hajaoneka muda mrefu akiwa ulingoni.

Anasema awali alikuwa akienda nchini humo kwa ajili ya kumtembelea mama yake mzazi kabla ya kuona kuwa kuna fursa za kupiga pesa akiwa huko.

“Wakati huo, mwanangu Boniface na Azenga walikuwa wakiishi huku na bibi yao, hivyo haikunipa ugumu, ingawa mke wangu Toshi (Azenga) aligoma kuhamia Msumbiji.”

Anasema mwanzo aliamua kurudisha mpira kwa kipa na kurudi kuishi na mama yake, akijipanga upya kwenye biashara hiyo ambayo ndiye alikuwa mwanzilishi kwenye eneo la Mueda.

“Watu wa huku hawakuwa wakiijua biashara hii na faida yake, hivyo

nilijikuta nikikusanya mzigo mkubwa kwa gharama nafuu, nilihamishia mashine yangu ya kusaga huku Msumbiji tayari kwa kuanza kazi,” anasema.

Aanza kupiga pesa

Cheka anasema baada ya muda mfupi alianza kupata mafanikio kwa kupiga pesa kutokana na biashara hiyo ambayo kwa jicho la kawaida inaonekana ni ya kimasikini.

“Nina uhakika wa kusaga hadi magunia 100 (ya chupa) kwa mwezi, kila gunia nikiuza si chini ya Sh55,000, hii ni biashara ambayo inaniingizia kipato kikubwa kushinda kile cha ngumi.

“Wakati naifanya Morogoro mwanzoni ndiyo imeniwezesha kujenga nyumba Kihonda nilikopangisha na Kilimahewa ambako inaishi familia yangu.” Anasema wateja wake wakubwa ni raia wa Kiasia wanaoishi Dar es Salaam, hivyo anafanya biashara ya masafa marefu kutoka Msumbiji hadi Dar es Salaam.

Hana mpango wa kurudi Bongo

Bondia huyo aliyewahi kuwa tishio nchini anasema hana mpango wa kurudisha majeshi nchini, kwani maisha yake sasa yatakuwa nchini Msumbiji.

“Naishi kihalali Msumbiji, niko nyumbani japo huwa naikumbuka Tanzania, lakini nilishaamua kuanza maisha mapya huku, nikirudi Tanzania labda kutembea.”.

Mipango ya ngumi

Cheka ambaye mara ya mwisho kupanda ulingoni ilikuwa Desemba 2018 alipochapwa na Abdallah Pazi (Dullah Mbabe) kwa Knock Out (KO), anasema baada ya pambano hilo wengi wanaamini kiwango chake kimeshuka, na siyo Cheka aliyekuwa akiwakung’uta mabondia wengi Bongo.

“Sijui nini kilitokea hadi nikapigwa KO na Dullah, binafsi mpaka leo bado siamini na nitaendelea kutoamini, ndiyo sababu nahitaji pambano la marudiano naye, kama akinipiga basi nitatangaza kustaafu ngumi rasmi,” anasema.

Bondia huyo wa uzani wa Super middle anasema licha ya kufanya biashara zake, lakini hajaacha kufanya mazoezi kwani anajifua na mbali na kutaka marudiano na Dullah, pia atacheza pambano lake la kwanza nchini Msumbiji baadaye mwaka huu kama ambavyo masha-biki wake nchini humo wamemuomba.

Safari ya maisha

Cheka alianza kujifunza ngumi akiwa kijana alipochukuliwa na promota Shomari Kimbau akitokea klabu ya ngumi ya Ngome ambako alikuwa akijifua.

Anasema alijifunza ngumi baada ya maisha kuwa magumu nyumbani kwao ambako alilelewa na mama wa kambo.

“Nikiwa najifunza ngumi, nilipata kazi ya kuzoa taka Manispaa ya Ilala, baada ya muda nilifikiria kuiacha ile kazi na kuondoka Dar es Salaam kwenda Morogoro kuanza maisha mengine.

“Nilikuwa na Sh20,000 nilipofika stendi sikuwa na pa kwenda, nikatafuta maboksi nikatandika pale nikalala, maisha yakaanza,” anasema.

Anasema siku iliyofuata alijiongeza kwa kuomba kuwa mfanya usafi katika stendi ya Msamvu, akakubaliwa na akatumia mwanya huo kukusanya chupa za plastiki, biashara ambayo aliifahamu akiwa Dar es Salaam akizoa taka katika Manispaa ya Ilala.

Baada ya miezi kadhaa alikutana na mabondia ambao aliwahi kucheza nao kwenye mashindano ya klabu bingwa Taifa ambayo yalifanyika Mwanza, enzi akiwa na timu ya Ngome ambao walimchukua na kwenda kuishi naye maskani kabla ya kukutana na kocha wa ngumi, Abdallah Salehe (Comando).

“Kocha nilikutana naye kwenye mashindano ya Mwanza, nilipokutana naye Morogoro, alikuja ninapoishi kabla ya kunichukua nikaishi kwake, nikaanza kutambulika kama mjukuu wa Abdul Salehe ambaye ni baba yake na kocha Comando.”

Anakumbuka biashara ya chupa aliiendeleza akiwa kwa kocha huyo ambaye alimpa eneo la kukusanyia bidhaa hiyo wakati huo Cheka akiwa anatembea mtaani kuokota chupa mwenyewe.

“Nilikusanya chupa hadi zikafika tani tano pale kwa Comando, hakuna aliyekuwa akifahamu umuhimu wa chupa pale Morogoro wakati ule, kuna Mhindi mmoja anaitwa Satia ni mfanyabiashara mkubwa wa chupa za plastiki Dar alipata habari zangu akanifuata Morogoro, nikamuuzia mzigo na kupata Sh2.5 milioni niliyoanzia maisha.

“Yule Mhindi alikuja kuwa rafiki yangu mkubwa na ndiye aliyeniuzia mashine ya kusaga chupa ambayo ninayo hadi sasa,”anasema

Anasema mkewe Toshi alikutana naye eneo la Msamvu mjini humo akiwa anafanya biashara ya chakula na yeye (Cheka) alikuwa ni mteja wake.

Cheka anasema katika maisha yake ya ngumi hatasahau hukumu ya miaka mitatu jela aliyohukumiwa Februari 2, 2015.

“Siku ya hukumu niliondoka nyumbani nikiwa tofauti, niligombana sana na mke wangu siku hiyo, nikamwambia sitaki nikuone mahakamani, nikaondoka, ila baadaye mke wangu alinifuata nyuma.

“Nilisomewa mashtaka yangu, hakimu akaniambia jitetee, siku hiyo sijui nilikuwaje nikamjibu hakimu fanya uamuzi wowote ambao mahakama inaona.

“Nilijibu kwa hasira, nadhani sababu niliona kama mimi ndiye nilikuwa nastahili kushtaki, kwani huyo aliyedai nimempiga ndiye alinifanyia mambo ya ajabu.

“Nilichukua fedha yangu ya pambano la Phil Williams nikampa na nyingine nilikopa benki ili tufanye biashara, siku nakwenda hakuna chochote kinachofanyika, hakuna pesa, nilipomuuliza akanijibu vibaya, kama binadamu nilipata hasira (nikampiga),” anasema Cheka.

Hata hivyo, hakukaa muda mrefu gerezani kabla ya kupewa hukumu ya nje ambayo ilimlzimu kufanya usafi katika ofisi ya Manispaa ya Morogoro ikiwa ni pamoja na kufyeka, kupalilia nyasi, kukata maua na wakati mwingine kufagia eneo linalozunguka manispaa hadi alipomaliza kifungo.