GSM balaa yatenga 1.5 billioni kuibomoa Simba

MASHABIKI wa Yanga sasa wana kila sababu ya kula na kushiba, kwani mdhamini wao kampuni ya GSM, imetangaza kurejea rasmi Jangwani na fasta mabosi wake wakaamua kutenga Sh 1.5 bilioni kwa ajili ya kubomoa utawala wa Simba katika Ligi Kuu Bara.

Kwa misimu miwili iliyopita, Simba ilijitengenezea ufalme wake kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na msimu huu wana kila dalili za kuubeba kwa mara ya tatu mfululizo na hilo mabosi wa GSM na wale wa Yanga waliomaliza tofauti zao wamebaini na kujipanga kwa msimu ujao.

GSM na Yanga jana waliweka hadharani makubaliano yao ya kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi ya ule uliokuwapo mwanzoni kabla ya hali kutibuka, lakini imefichuka wametenga bajeti nzito kwa ajili ya kurejesha heshima kwa klabu yao kwa msimu ujao wa 2020-2021.

Jana mchana Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Mhandisi Hersi Said walikuwa na mkutano maalum ambapo wadhamini hao walitangaza uamuzi wa kurejea rasmi wakivunja uamuzi wao wa awali.

Awali, GSM walijiondoa katika kutekeleza majukumu ya nje ya mkataba wao wa udhamini ikiwa ni kushiriki katika kuisajilia timu hiyo, kulipa wachezaji posho na mishahara na kugharamia kambi ya kikosi chao.

Hata hivyo, Hersi jana alisema wao bado ni familia ya Yanga na kwamba wanarejea kuhakikisha wanaendeleza juhudi za kuirudishia nguvu timu hiyo.

FUNGU LA USAJILI

Wakati pande hizo mbili zikiweka wazi makubaliano hayo nyuma yake ikafichuka kwamba katika kikao cha pamoja cha usuluhishi za pande hizo kilichofanyika mapema wiki hii, GSM iliweka mezani fungu la Sh 1.5 bilioni kuhakikisha wanaijenga timu yao na kubomoa utawala wa Simba.

Taarifa kutoka ndani ya mabosi hao ni kwamba kiasi hicho kitatumika katika kulipa ada za usajili wa timu hiyo ambazo ni madeni ya nyuma pamoja na wale wapya.

Pia imeelezwa zitatumika katika kulipa gharama ya wachezaji ambao watavunjiwa mikataba yao sambamba na kutumika kusajilia wachezaji wapya.

“Jamaa wanataka kujenga timu ya kweli itakayoshindana kwa dhati lakini pia wanataka kuona kama kuna wachezaji wataachwa wanaondoka kwa amani kulingana na mikataba yao,” alifichua mmoja wa mabosi wa klabu hiyo.

Katika mkutano wa jana, Hersi alithibitisha hilo kwa kusema; “Tunahitaji kuwa na timu yenye nguvu. Kwa miaka mitatu sasa tumekuwa tukikosa mataji. Hili GSM tunaona lifike mwisho. Msimu ujao tunataka kuona mataji yetu yanarudi yote.”

“Dhamira yetu itakuwa moja kwamba tutasajili timu bora itakayokwenda na hadhi na ushindani wa ligi, tutawasiji wachezaji bora ambao watakuja kuungana na hawa watakaobaki lakini pia tutawabakiza wachezaji bora ambao tunaona bado tunahitaji huduma zao.”

Katika ripoti ya Kocha Luc Eymael, Mwanaspoti inafahamu Mbelgiji huyo ametaka kusajiliwa wachezaji wanne wa kigeni wakiwemo mastraika, mawinga, viungo wa kati.

Katika usajili huo, Mwanaspoti inafahamu kwamba GSM kama sio leo basi kesho watafungua sanduku la fedha kwa kumalizana na kiungo na nahodha wao Papy Tshishimbi ambaye mpaka sasa kuna uwezekano wa asilimia 85 kusalia katika kikosi hicho.

MSIKIE MSOLA

Naye Mwenyekiti wa Yanga, Dk Msolla alisema mabadiliko ndani ya klabu hiyo haliepukiki na tayari wameweka mipango kamili ya kulianzisha jambo hilo walilopanga mchakato wake uanze mwezi ujao na wamefurahi kuona GSM wameonyesha nia katika mchakato huu.

Dk Msolla alisema tayari wameanza kuunda kamati nyingine mpya kama (Kamati ya Mabadiliko), itakayokuwa na Wajumbe wa Yanga wenye uweledi na suala hilo lakini watachanganyika wa wajumbe wengine kutoka GSM.

“Tutaunda kamati nyingine ya pili ambayo itakuwa kamati ndogo ya masuala ya kikatiba ambayo wataipeleka katika matawi ya nchi nzima ili nao wapate kuisoma na kuelewa jambo gani ambalo wanakwenda kulifanya katika klabu yao na kutoa idhini kuwa lifanyike kwa mfumo upi,” alisema.

“Pia katika kampeni suala la kubadilisha mfumo wa kuendesha klabu lilikuwa moja ya kipaumbele changu, lakini tunawakaribisha watu wa aina yoyote ambao wana uwezo wa kuisadia Yanga. Uongozi upo tayari kwani dhamira yetu ni kuhakikisha msimu ujao tunakuwa mabingwa, hivyo lazima tushirikiane.”