GSM warejea kwa kishindo Yanga kuanza na ujenzi wa uwanja Kigamboni

WANACHAMA na mashabiki wa Yanga waliokuwa wakiishi kwa presha tangu waliposikia, mmoja wa wadhamini wao, Kampuni ya GSM ametaka kujiengua kwenye shughuli zilizopo nje ya mkataba na klabu yao, sasa wale na kushiba tu, kwani kila kitu kipo sawa.

Ndio, mdhamini huyo baada ya kuipokea barua ya uongozi wa Yanga iliyotumwa kwao Ijumaa iliyopita na wenyewe kuipata Jumatatu ikiwaomba msamaha kwa yaliyotokea na kuelezwa hatua zilizochukuliwa, mabosi wa kampuni hiyo wameridhia kuanza upyaa.

Kama umesahau ni kwamba Machi 24, GSM waliuandika uongozi wa Yanga kwamba wanataka kujiondoa kwenye shughuli za usajili, kulipa posho na mishahara ya wachezaji sambamba na kambi ya timu kwa sababu wanaonekana kama wanaiingilia Kamati a Utendaji ya klabu. Fasta viongozi wa klabu hiyo waliamua kuitisha kikao kizito cha siku mbili kabla ya Ijumaa jioni kutangaza kujiuzulu kwa wajumbe watatu, Shija Richard, Rodgers Gumbo na Said Kambi, huku ikiwasimamisha Salim Rupia na Frank Kamugisha na kisha kuwaandikia barua mabosi wa GSM.

Viongozi wa Yanga walilazimika kuchukua hatua hiyo baada ya kutishwa na joto la wanachama wao walioanza kuwaandama kwa tishio hilo la kujitoa kwa GSM ambaye tangu atue klabuni hapo amewapunguzia machungu waliyokuwa nayo kwa chama lao kuondokana na hali ya kuwa ombaomba.

Jana Mwanaspoti liliamua kuwasaka mabosi wa GSM kujua kama wameshaipata barua na nini msimamo wao, ndipo wakafunguka kila kitu kimeisha na wanarejea klabuni wakiwa na mambo makubwa zaidi ya yale waliyokuwa wakiyafanya awali na kuzinguliwa na baadhi ya wajumbe.

Mmoja ya vigogo wa kampuni hiyo aliyeomba kuhifadhiwa jina, alithibitisha kuwa wamesamehe kila kitu baada ya kuombwa radhi na kufahamishwa hatua zilizochukuliwa na sasa wanaanza mambo upya wakidai wamekuja kivingine ili Yanga izidi kutakata. Awali mmoja wa viongozi wa Yanga alithibitisha GSM kuwasamehe na wamepania kufanya makubwa ikiwamo kuanza na ujenzi wa hosteli ambao ulikuwa mpango wao wa awali, sambamba na uwanja wa mazoezi kwa timu mbali na kuhakikisha klabu inaingia kwenye mfumo wa kisasa kwa kuwaletea mabosi wa La Liga. Mtoa habari huyo alisema tayari maongezi yanaendelea kuhusu mfumo mpya wa uwekezaji ambapo mazungumzo yalikuwa yameanza na kampuni ya La Liga ila kutokana na kujiondoa kwake zoezi hilo likawa limesitishwa, baada ya kukubali kurejea kila kitu kinaenda sawa.

“Hili la mfumo mpya ilikuwa janga kubwa endapo angeendelea na msimamo huo, kwani mtu anajitolea milioni 200/- kuwaleta La Liga hapa nchini ndani ya miezi mitatu wangemaliza kazi hiyo, na hapo awali alishamleta Mreno kwa gharama zake, japo walishindwana halafu mtu kama huyu watu wanamkera,” kilisema chanzo hicho.

Pia mtoa habari huyo alisema, mchakato wa ujenzi wa uwanja na hosteli eneo lao la Kigamboni na wenyewe utaendelea kama kawaida ili timu yao msimu ujao iwe na uwanja wake wa mazoezi kama wenzao Simba walivyofanya hivi sasa na kujikuta wakipunguza gharama za kulipia viwanja hivyo kwa saa Sh 500,000.

“Kama sio kumkera tayari angeshaanza kuonyesha vitu kule Kigamboni, lakini hakijaharibika kitu cha msingi ametusamehe na kurejesha moyo wake, na sasa amekuja kivingine zaidi, nakwambia usajili utakaofanyika Yanga utakuwa wa aina yake,” aliongeza na kudai kwa sasa wameanza kuangalia usajili wa wachezaji wanaomaliza mikataba yao kama bado Kocha Mkuu, Luc Eymael anawahitaji, ili waongezewe ili wasiondoka.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi walisema wangependa kuona usajili ukisimamiwa zaidi na klabu na GSM watashirikishwa kwenye masuala ya kifedha kwa nia ya kuhakikisha viongozi wanakuwa na sauti kwa wahusika, ili hata likitokea la kutokea wajue namna ya kujibeba.

YANGA WATUPIANA MPIRA

Hata hivyo viongozi wa Yanga walipotafutwa ili kuthibitisha taarifa hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela na Ofisa Habari, Hassan Bumbuli walisema suala hilo anayeweza kulizungumzia ni Mwenyekiti wa klabu, Dk Mshindo Msolla.

“Mwenyekiti ndiye msemaji wa jambo hilo, yeye ndiye mwenye power au Katibu Mkuu, kwangu mimi liko nje ya uwezo wangu na bado halijashuka kwangu, hivyo siwezi kusema lolote,” alisema Bumbuli, wakati Mwakalebela alisema suala hilo litazungumzwa na Mwenyekiti waou kwani ni suala zito na nyeti. Dk Msolla alipotafutwa na Mwanaspoti alisema kwa ufupi kwamba yuko bize na asingeweza kuzungumza lolote na kuomba atafutwe siku nyingine.

“Nitafute siku nyingine, ila kwa sasa nipo bize sana, sitaweza kuzungumza chochote ndugu yangu,” alisema Dk Msolla ambaye aliingia madarakani na wenzake Mei 5, mwaka jana.