Gadiel, Tshabalala waibua mjadala mzito Simba SC

Dar es Salaam. Wakati Simba jana ilimtambulisha rasmi beki mpya, Gadiel Michael, baadhi ya makocha wametoa maoni kuhusu ushindani wa namba utakavyokuwa baina yake na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ katika kikosi hicho msimu ujao.

Gadiel aliyejiunga Simba kwa mkataba wa miaka miwili, anacheza nafasi sawa uwanjani na Tshabalala ambaye ni nahodha msaidizi na huenda wakampa wakati mgumu Kocha Patrick Aussems kupata chaguo lake la kwanza.

Ingawa Gadiel na Tshabalala pia wana uwezo mzuri wa kucheza nafasi ya winga wa kushoto, lakini katika vikosi vyao hadi timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ wamekuwa wakitumika kama mabeki wa pembeni.

Gadiel alipokuwa Yanga alikuwa chaguo la kwanza kwa Kocha Mwinyi Zahera katika nafasi ya beki wa kushoto kama alivyokuwa Tshabalala chini ya Aussems.

Katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike alimpanga beki Gadiel katika mechi mbili dhidi ya Senegal waliofungwa mabao 2-0 na Kenya waliolala 3-2, wakati Tshabalala alicheza mechi ya mwisho waliochapwa 3-0 dhidi ya Algeria.

Kauli ya Minziro, Rishard

Wakati baadhi ya wadau wakijiuliza namna ambayo benchi la ufundi la Simba litawatumia bila kuathiri vipaji vyao, Kocha Fred ‘Felix’ Minziro alisema kocha ndiye atakuwa na uamuzi wa kupanga mchezaji wa kuanza kulingana na ubora na aina ya mchezo.

“Kocha anaweza kutumia mbinu nyingine ya kumpanga mmoja winga na mwingine beki hapo ndipo utaona umuhimu wa mchezaji kujua kucheza nafasi nyingi uwanjani.

“Vinginevyo lazima mmoja aanzie benchi ingawa Gadiel na Tshabalala uwezo wao ni kama unafafana, hivyo kocha ana nafasi ya kuangalia yupi amuanzishe,”alisema Minziro.

Kocha wa Polisi Tanzania, Selemani Matola alisema kati ya Gadiel au Tshabalala atalazimika kuanzia benchi.

“Gadiel na Tshabalala kila mmoja ana uwezo wake, kilichopo ni kocha kuwatumia kwa kupishana, awali alikuwepo Asante Kwasi (ameachwa) na kocha alikuwa akiwapishanisha japo Tshabalala alifanya vizuri zaidi ya Kwasi,” alisema Matola.

Kocha wa Prisons ya Mbeya, Mohammed Rishard ‘Adolf’ alisema usajili wa Gadiel unamrahisishia kazi Aussems. “Vita ya namba itakuwa kali, kila mmoja bila shaka hatapenda kupoteza nafasi na wote watajituma kwa ubora wa hali ya juu kitendo ambacho kitampa nafasi Aussems kuamua yupi aanze kikosi cha kwanza na nani aanzie benchi.

“Kati yao atakayeshuka kiwango atapoteza namba, lakini wote ni mabeki wazuri na ujio wa Gadiel utampa changamoto Tshabalala. Itakuwa ni vita baina yao lakini yenye manufaa kwa kocha na klabu” alisema Adolf.

Juzi akizungumza na gazeti hili, Gadiel alisema hana hofu ya kupata namba kikosi cha kwanza kwa kuwa ana kiwango bora.