Gadiel asaini Simba miaka mwili, Yanga roho nyeupe

Tuesday July 9 2019

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam. Simba imemtambulisha beki, Gadiel Michael leo Jumanne Julai 9, 2019saa 7:00 mchana baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na mabingwa hao.

Usajili wa Gadiel umemaliza tetesi za muda mrefu kuwa anajiunga na Simba akitokea Yanga akiwa mchezaji huru kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji Ibrahimu Ajibu.

Mbali ya Simba kumtambulisha Gadiel pia jina lake tayari lilikuwa katika orodha ya wachezaji wao iliyopelekwa CAF tayari kwa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Akizungumzia usajili wake Simba, Gadiel alisema atapambana ili kupata namba kwenye kikosi cha kwanza cha Mabingwa hao wa Ligi Kuu.

Gadiel anacheza beki namba mbili nafasi anayocheza Mohamed Hussein 'Tshabalala' alisema nguzo pekee itakayompa namba kwenye kikosi cha kwanza ni kujituma na kujiamini huku akitolea mfano wakati anatoka Azam FC kwenda Yanga aliamini katika kujituma.

"Kikosi cha Simba kina wachezaji wenye uwezo na kiwango bora, natarajia ushindani lakini hiyo ndiyo fursa kwangu ya kufanya nijitume zaidi," alisema Gadiel ambaye amejiunga na Simba akitokea Yanga.

Advertisement

Gadiel alisema atapambana kuhakikisha anafanya kitu ambacho kitaacha alama kwenye soka la Tanzania.

"Si kitu kidogo kupata nafasi ya kucheza Simba, Yanga wala Azam, wapo wachezaji ambao wanatamani kuzichezea na bado hawajafanikiwa, nitapambana kwa kadri nitakavyoweza Simba ili iwe njia ya mimi kucheza nje ya nchi," alisema.

Akiizungumzia timu yake ya zamani ya Yanga, Beki huyo alisema mabingwa hao wa kihistoria imempa mwanga katika maisha yake ya mpira na kusisitiza kwamba klabu hiyo ya Jangwani itabaki kwenye kumbukumbu yake.

"Kikubwa mmashabiki walionisapoti nikiwa Yanga wanapaswa kutambua kwamba mpira ni kazi inayofanya maisha yangu yaende, nahitaji changamoto mbalimbali za kufanya kiwango changu kizidi kuwa juu na hatimae niweze kwenda kucheza soka nje ya nchi," alisema Gadiel.

Kuhusu madai ya Simba kuifuata Yanga ili kumruhusu beki huyo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema hawajaka na Simba kwa sababu ni mchezaji huru.

"Simba hawajatufuata na kutuomba tuwaruhusu wamsajili Gadiel CAF na sisi tukawaruhusu, sio kweli, Gadiel yuko huru hana mkataba na Yanga tangu Juni 30," alisisitiza Mwakalebela.

Nyota huyo aliyewahi kuichezea Azam ni miongoni mwa wachezaji waliotajwa kwenye usajili wa Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Advertisement