Galatasaray 0-1 Real Madrid: Hazard akosa bao la msimu mashabiki wamtolea uvuvi

Muktasari:

Real Madrid imefufua matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo baada ya kutopata ushindi katika mechi mbili zilizopita.

Istanbul, Uturuki. Licha ya nyota Eden Hazard kukosa bao baada ya kupiga kiki iliyogonga mwamba, Real Madrid ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Galatasaray katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Real Madrid imefufua matumaini ya kusonga mbele katika mashindano hayo baada ya kutopata ushindi katika mechi mbili zilizopita.

Kocha Zinedine Zidane ameshusha presha baada ya kufungwa katika mchezo uliopita na Mallorca katika mchezo wa Ligi Kuu Hispania.

Pia Zidane ameokoa kibarua chake kwani angefungwa mjini Instabul angetupiwa virago.

Hazard alifanya kazi nzuri ya kuwatoka mabeki na kipa wa Galatasaray, lakini shuti lake alilopiga kwa mguu wa kulia iligonga mwamba kabla ya kurejea uwanjani na kuokolewa na mabeki.

Hazard aliyenunuliwa kwa fedha nyingi akitokea Chelsea katika usajili wa majira ya kiangazi, alipiga kiki hiyo akiwa umbani wa hatua sita tu.

Toni Kroos aliipa Real Madrid bao hilo dakika ya 18 na kuishusha presha na Zidane ambaye tangu kuanza msimu huu amekuwa kikaangoni.

Real Madrid imefikisha pointi tano katika msimamo wa Kundi A ikiwa na pointi tano nyuma ya vinara Paris Saint Germain (PSG).

Timu hiyo ilianza vibaya kampeni ya kuwania ubingwa kwa kucharazwa mabao 3-0 dhidi ya PSG kabla ya kutoka suluhu na Bruges matokeo ambayo yalimuweka matatani Zidane.