Giroud amaliza gundu Ufaransa

Monday September 10 2018

 

Paris, Ufaransa. Sahau mshambuliaji kinda wa Ufaransa, Kylian Mbappe kuendeleza cheche zake katika angaza kimataifa Olivier Giroud, aliyecheza mechi zote za fainali za Kombe la Dunia bila kupata bao hata moja, jana alimaliza gundi kwa kuifungia nchi yake.

Mbappe alifanya kweli baada ya kuifungia Ufaransa bao la kuongoza katika dakika ya 14, ikiilaza Uholanzi kwa mabao 2-1, katika mchezo wa pili kwa mabingwa hao wa Dunia katika mashindano ya Uefa Nations League, katika mchezo wa kwanza walitoka sare na Ujerumani na hivyo kukalia kiti cha uongozi wa kundi lao.

Uholanzi ambao walizikosa fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia, walikianza kipindi cha pili kwa nguvu na kufanikiwa kusawazisha bao katika dakika ya 67 likifungwa na Ryan Babel.

Hata hivyo matumaini ya kuondoka walau na pointi moja ugenini yalishindikana baada ya mshambuliaji wa Chelsea anayelaumiwa kwa kushindwa kufunga Olivier Giroud, kumaliza mkosi alipoifungia Ufaransa bao la ushindi katika dakika ya 74.

Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps, aliamua kufanya mabadiliko ya baadhi ya wachezaji akiwaacha wale waliotoka sare ya bila mabao na Ujerumani ukiondoa kipa majeruhi, Hugo Lloris, Kocha huyo alipanga kikosi kile kilichocheza fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Croatia.

Uholanzi itaikaribisha Ujerumani Jumamosi hii kabla ya Ujerumani kuifuata Ufaransa Jumanne ya Oktoba 16 mwaka huu.

Matokeo mengine ya mechi za michuano hiyo zilizopigwa jana yalikuwa, Ukraine 1 vs Slovakia 0,    Denmark 2 vs Wales 0, Bulgaria 1 vs  Norway 0, Georgia 1 vs Latvia, Macedonia 2 vs Armenia 0 Cyprus 2 vs Slovenia 1 na Liechtenstein 2 vs Gibraltar 0.

Advertisement