Golota kuona Kombe la Dunia 2018 uraiani

09: Ni namba aliyokuwa akicheza Golota akiwa Simba, Taifa Stars

Muktasari:

  • Ni baada ya kumaliza kifungo chake Uhabeshi.

Ethiopia. Mshambuliaji wa zamani wa Simba anayetumikia kifungo cha miaka saba na nusu jela nchini Ethiopia, Joseph Kaniki ‘Golota’, huenda akazitazama fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Russia akiwa uraiani.

Golota alianza kutumikia kifungo cha miaka saba na nusu jela mwaka 2012 baada ya kukutwa na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya akiwa safarini kwenda Ulaya.

Mshambuliaji huyo alikamatwa sanjari na bondia wa Tanzania, Mkwanda Matumla wakiwa katika harakati za kuunganisha ndege kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Addis Ababa.

Ofisa wa Ubalozi wa Tanzania nchini  Ethiopia anayeshuighulikia Amani na Usalama, Sevike Ndatta, alisema Golota na Mkwanda wamebakiza miaka miwili na nusu ya kutumikia adhabu zao.

Ndatta alisema kwa hesabu za kifungo, wanamichezo hao wa Tanzania wamebakiza miaka miwili na nusu, hivyo katikati ya 2017 watakuwa huru.

“Kaniki (Golota) na Mkwanda (Matumla ni miongoni mwa Watanzania sita wanaotumikia kifungo nchini Ethiopia, wakati wengine wawili wakiwa mahabusu,” alisema Ndatta.

Ofisa huyo aliongeza kwamba Golota anaungana na Watanzania wote wanane  katika kesi inayofanana ya kuhusika na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia Uwanja wa Ndege wa Addis Ababa.

“Sheria za usafirishaji na matumizi ya dawa za kulevya ni ngumu katika nchi zote. Tunachofanya kama ubalozi ni kutoa msaada ambao upo ndani ya uwezo wetu, tunafika mara kadhaa kuwaona na kuwapa mahitaji,” aliongeza ofisa huyo wa kibalozi.

Ndatta alisema, mshambuliaji huyo amepewa msaada mkubwa wa  kuhakikisha anatoka, lakini bila mafanikio kutokana na ushirikiano mdogo wanaoupata wanapopiga namba za watu anaodai ni ndugu zake kusikia kuwa wanazungumza na wa Serikali.

Aidha, Ndatta alitoa wito kwa vijana wa Kitanzania wasikubali kujiingiza kwenye biashara ya dawa za kulevya kutokana na ukali wa adhabu yake pindi wanapotiwa hatiani.