Gor Mahia yatangazia vita Noir, Pollack atamba kwa sare

KOCHA mpya wa Gor Mahia, Steven Pollack kaanza kibarua chake kwa chocha.

Baada ya kutoka sare tasa dhidi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Burundi, Aigle Noir FC kule kwao Bujumbura kwenye mechi ya raundi ya kwanza ya kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya CAF Champions League, sasa Pollack kasema majamaa wakija Nairobi, watawanyoosha propa.

Timu hizo zitacheza uwanjani Kasarani kwenye mechi ya marudio na Gor watakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kwamba hawatoki sare ya magoli. Kwa kifupi, Gor wanahitaji ushindi wa aina yoyote kufuzu kwa raundi ya pili ya mchujo.

Licha ya kufahamu mtihani huo mgumu, kocha Pollack aliyelazimika kusafiri na timu ndogo ya wachezaji 15 badala ya 18 kuelekea Bujumbura kutokana na wengi wao kukumbwa na utata wa vibali vya usafiri, kasisitiza kuwa Aigle wataumia mjini Nairobi.

“Nafikiri mambo yalikwenda vizuri tu, hatukuwa kwenye hatari ya kupoteza toka mwanzo. Licha ya kuwa na upungufu wa wachezaji bado tulipata ujanja wa kuwadhibiti,” Pollack alianza kwa chocha.

Na sasa tayari anasema ana mpango wa namna atakavyowazima Aigle watakapotua Nairobi baada ya wiki moja hivi.

“Kwa sasa ni kipindi cha mapumziko na tayari tushajua staili yao ya mchezo, tutajiandaa vizuri nyumbani, wakija tuwanyoroshe,” Pollack akaongeza.