Guardiola aonya wachezaji England kuumia

Muktasari:

  • Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesema England itapata pigo la wachezaji wengi kuumia kutokana na mfumo usiofaa wa ratiba katika mechi za mashindano nchini humo.

 London, England. Pep Guardiola ameonya kuwa wachezaji wa England wataendelea kuumia kutokana na idadi kubwa ya mechi wanazocheza.

Guardiola ametoa kauli hiyo baada ya washambuliaji wawili tegemeo wa England nahodha Harry Kane na Marcus Rashford kuumia vibaya.

England inaweza kuwakosa nyota hao katika mechi za Ulaya kwa kuwa watakuwa nje ya uwanja muda mrefu kabla ya kurejea uwanjani.

Kocha huyo wa Manchester City alisema wachezaji wa England wanatumika zaidi katika mechi za Ligi Kuu na mashindano mengine ndani ya msimu mmoja kulinganisha na nchi nyingine.

Alisema kwa muda mrefu amepigia kelele jambo hilo lakini hakuna hatua zinazochukuliwa, hivyo klabu zitegemee kuwakosa nyota wake wengi kutokana na majeraha.

Wakati Kane wa Tottenham Hotspurs atakuwa nje ya uwanja wiki 12 , Rashford atakosa mechi za Manchester United miezi mitatu.

“Pole kwa Kane na Rashford. Ni pigo kubwa na hii inatokana na mfumo wa ligi ulivyo, lakini tumekuwa tukilalamika bila mafanikio, tutegemee idadi kubwa ya wachezaji kupata maumivu,”alisema Guardiola.

Kocha huyo alisema wachezaji England wanacheza mechi nyingi kulinganisha na Ujerumani au Hispania. Guardiola alisema idadi kubwa ya mechi zinachezwa katika kipindi cha majira ya baridi.