HISIA ZANGU: Ilikuaje Morrison miezi sita, Yikpe miaka miwili?

Aliyewaloga Yanga ni nani? Ilikuwaje wakampa Benard Morrison mkataba wa miezi sita, halafu wakampa Yikpe Gnamien mkataba wa miaka miwili? Nani aliwaroga Yanga? Kuna pepo mbaya alipita wakati walipofanya maamuzi haya.

Walau sasa Yanga wanaweza kupumua baada ya kufanikiwa kumpatia mkataba wa miaka miwili Morrison. Lakini tujiulize ilikuwa walifanya hii faulo hapo awali. Kuna kitu kinanishangaza sana. Hakitaacha kushangaza.

Yanga walimpa mkataba wa miezi sita Morrison bila ya kumuona. Nadhani walitazama video zake. Hawakuwahi kumuona uwanjani akicheza. Wakaamua kumpa mkataba. Ghafla akageuka kuwa mchezaji mzuri na tegemeo klabuni.

Licha ya kufanya masikhara ya kuupanda mpira lakini Morrison huwa anafanya mambo mengi ya msingi uwanjani. Amenyimwa penalti za kutosha lakini tayari amefunga. Amepika mabao. Unajiuliza kwanini Yanga walihatarisha namna hii.

Nasikia Simba walikuwa wanamnyatia. Lakini kwa aina ya mkataba wake basi kumbe wajanja wa mjini akina Simba na Azam wangeweza kumsainisha mkataba wa awali muda wowote ule tangu alipotua Yanga. Mchezaji anaruhusiwa kuongea na klabu nyingine mkataba wake unapobakiza miezi sita. Kumbe Morrison angeweza kuanza kuongea na Simba au Yanga muda mchache tu baada ya kusaini Yanga.

Lilikuwa ni kosa la kiufundi. Sijui kwanini hawakumuamini. Nadhani akili yao ilikuwa inawaambia wasiingie mkenge. Lakini ghafla wakajikuta wana dhahabu mkononi. Wenzetu huwa hawafanyi kosa la kiufundi kama hili. Kama unadhani hili ni kosa basi subiri. Uvivu wa Yanga kutomtazama Morrison vema alikotoka na kujiridhisha kiwango chake nusura uwagharimu. Lakini hapo hapo inashangaza kuona kuna mchezaji walipata nafasi ya kumtazama na wakaamua kumpa mkataba wa miaka miwili licha ya ubovu wake. Yikpe.

Alifanya uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akiwa na umbo kama la wacheza kikapu wa Marekani. Awali Yanga waligoma kuingia mkenge moja kwa moja. Akatishia kuondoka. Wakati huo Yanga ilikuwa ina shida ya washambuliaji kwa sababu ilishaachana na washambuliaji wake akina Juma Balinya.

Yanga wakamlazimisha asafiri mpaka Mbeya akaungane na timu ili watazame kiwango chake kabla ya kumpa mkataba. Ni kweli Yanga walimtazama. Mpaka sasa najiuliza, walitumia jicho gani? walitumia akili gani?

Sioni kitu cha ziada ambacho mshambuliaji huyu wa Ivory Coast anacho. Ni mshambuliaji wa kawaida hasa. Afadhali Yanga wangemchukua Paul Nonga kutoka Lipuli. Kuna wakati Nonga alishinda kutamba Yanga ni kwa sababu nafasi yake kulikuwa na Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Amis Tambwe waliokuwa moto.

Kwa Yanga hii, afadhali uwe na Paul Nonga au Reliant Lusajo wa Namungo kuliko Yikpe. Yanga waliona nini kwake? Mshambuliaji kama yeye na umbo lile, na uzito ule, anaweza kukosa mambo mengi lakini akawa mfungaji mzuri. Kwake sioni kama anajipanga vizuri kwa ajili ya kuziona nyavu. Sioni kama anajua kukimbia vema nyuma ya mabeki. Sioni kama anaweza kuulinga mpira vema kama baadhi ya washambuliaji wenye maumbo makubwa kama akina Olivier Giroud wanavyofanya.

Binafsi nina tabia ya kuwavumilia wachezaji na kuwapa muda lakini kwa Yikpe uzalendo umenishinda. Alionyesha vitu gani mazoezini mpaka wakaamua kumpa mkataba wa miaka miwili? Upotevu wa pesa usio na sababu.

Walau angekuwa na kitu kimoja tu cha ziada ambacho kingempa nguvu mtu aliyepiga dili la kumpeleka Yanga lakini hata hicho kitu kimoja hana. Walau David Molinga anaweza kuwa na kitu cha ziada kuliko Yikpe. Anafunga.

Wakati mwingine kuna sababu za mazingira tu zinazoweza kusababisha muachane na mchezaji. Kwa mfano, mchezaji kutoka taifa la Ivory Coast, mwenye umbo lile, mwenye miaka 25, kama kweli anajua mpira kwanini acheze Tanzania? Kwanini Gor Mahia imruhusu kuondoka kwa urahisi vile?

Kama angekuwa na kitu cha ziada nadhani angekuwa mbali kwa sasa kwa namna ambavyo kaka zake akina Didier Drogba walishamuandalia mazingira ya kutamba. Taifa lake ni chati tosha kwake kufika mbali. Ukiona yupo ukanda huu ujue kuna jambo.

Kwa kifupi, haya yote mawili yametokana na klabu zetu kukosa mfumo imara wa kunasa wachezaji. Wazungu wanaita scouting. Kama Yanga ingekuwa imewatazama kwa muda mrefu wachezaji wote hawa wawili, Morrison na Yikpe basi kwanza wasingempa Yikpe mkataba kabisa, na hapo hapo wasingempa Morrison mkataba wa miaka miwili. Wangempa mkataba mrefu.

Hivi mashabiki wanawaelewa viongozi wao kwa kumpa mkataba wa miaka miwili Yikpe? Hivi mashabiki wangewaelewa viongozi wao kama Morrison angeenda Simba baada ya miezi sita tu? Na ndio maana tunasisitiza viongozi kuzitazama Ligi mbalimbali wakati michuano inaendelea ili wasiingie mkenge wakati wa uhamisho unapowadia.

Kwa Yikpe Yanga wameliwa. Na hasa unapozingatia kwamba Yanga walikuwa wametoka kuachana na washambuliaji wenye nafuu kuliko yeye. Hauwezi kumlinganisha Balinya na Yikpe. Wala hauwezi kumlinganisha na Sidney.