HISIA ZANGU: Yanga ya Kamusoko Orijino na Simba ya Chama

ALIYEWAROGA Simba na Yanga nadhani alishakufa miaka mingi iliyopita. Nadhani kabla yule Gavana wa mwisho wa kiingereza, Richard Turnbull hajamkabidhi Mwalimu Nyerere uhuru wake ule mwaka 1961. Kwanini Simba na Yanga hazitambi pamoja?

Kuna mtu nadhani aliwaroga Simba na Yanga wasitambe pamoja. Huwa haiwezi kutokea. Ni ngumu kwao kucheza mechi ambayo haina kibonde (Underdog) mtarajiwa. Mechi ya mwisho baina yao ilikuwa aibu zaidi. Yanga walizidiwa kila kitu na Simba.

Isingekuwa hivyo miaka michache kabla ya hapo. Yanga na utajiri wao walikuwa wanatokea Uturuki au Afrika Kusini wakiwa wamekamilika. Wakiwa na maringo mengi. Wakiwa wanalala katika hoteli ya hadhi ya nyota tano usiku mmoja kabla ya mechi.

Na sasa nimeikumbuka Yanga iliyopita miaka michache iliyopita. Yanga ya Donald Ngoma, Simon Msuva ule upande wa kulia, Thabani Kamusoko pale katikati. Haruna Niyonzima. Juma Abdul akitokea kulia na zile krosi zake. Obrey Chirwa alianza kwa kusuasua lakini baadaye akawa hashikiki. Amis Tambwe akawa hatari sana.

Yanga ile imepishana na Simba hii. Jambo hili limetokea kwa miaka nenda rudi. Simba wakiwa wazuri basi watapishana na Yanga iliyokuwa nzuri. Yanga wakiwa wazuri basi watapishana na Simba iliyo nzuri. Mara nyingi huwa haiwi ndani ya uwanja tu, hadi nje ya uwanja kunakuwa na migogoro.

Kama Simba hii inayotisha ya akina Meddie Kagere, Emmanuel Okwi, John Bocco, Clatous Chama na wengineo ingekutana na Yanga ya akina Ngoma nadhani tungeshuhudia pambano kali la soka. Ingekuwa vipi Kamusoko katika ubora wake na Chama wa leo katika ubora wake?

Ile Yanga iliyomfunga Al Ahly 1-0 katika Uwanja wa Taifa ingecheza na Simba iliyomfunga Saoura 3-0 katika uwanja huo, nadhani mechi yao ingekuwa ya kusisimua sana. bahati mbaya ni nadra kupata mechi za aina hii.

Mara nyingi mechi za Simba na Yanga zinabebwa na kelele nyingi lakini ni nadra kushuhudia ubora mwingi wa timu kupishana katikati ya uwanja. Kama Kamusoko aliye bora angekutana na Chama wa leo si ajabu tungeshuhudia marudiano ya mechi za mwanzoni mwa mwaka 1990 wakati Hamis Thobias Gaga ‘Gagarino’ alipokuwa anakumbana na Athuman China katikati ya uwanja.

Bahati hiyo imetoweka kwa sababu tajiri wa Yanga. Yusuf Manji ameondoka Jangwani baada ya kupata matatizo na Serikali. Bahati hiyo imeondoka kwa sababu Yanga inataka kuchagua viongozi ambao nina shaka kama wanaweza kutia pesa katika Yanga kama Manji alivyofanya.

Naungalia uchaguzi wa Yanga na kujiuliza. Wanaogombea wanakwenda kuvaa viatu vya Manji kwa maana ya uwekaji pesa katika timu au wanakwenda kwa ajili ya kuandaa mazingira ya klabu yao kupitia katika mabadiliko na kurudisha watu wa aina ya Manji katika sura tofauti ya uwekezaji ndani ya klabu?

Lakini ndivyo inavyotokea. Kuna mdudu wa nuksi lazima atatembelea Yanga au Simba pindi mmoja wao akiwa juu. Njia pekee ambayo tunaweza kumfuta mdudu huyu ni klabu hizi kuendeshwa kisasa na kuingia katika mfumo ambao Simba wameingia.

Mfumo huu kwa kiasi kikubwa unaweza kuzifanya Simba na Yanga zote zitambe kwa wakati mmoja. Katika ligi bingwa lazima awe mmoja lakini haimzuii mwingine kutamba. Tupo katika nyakati ambazo kuna michuano mingi ambayo inatoa fursa kwa timu tofauti ndani ya Ligi Moja kutamba.

Ingekuwa jambo la kufurahisha kama Simba ingefika fainali za Afrika na Yanga ingefika fainali za kombe la Shirikisho. Ubabe wa Yanga na Simba haupaswi kuishia katika ligi tu. kama klabu zote mbili zingeendeshwa katika mifumo ya kisasa nadhani wote wangeweza kutamba kwa pamoja na kumfukuza mchawi ambaye anadaiwa kuziroga klabu hizi.

Bahati nzuri zaidi ni kwamba wachezaji wazawa wangeendelea kukomaa japo kwa uchache wa nafasi zao kwa sasa dhidi ya wale wa kigeni ambao wanaonekana kutamba katika klabu kubwa. Huwa inasaidia wakati mwingine. Mafarao wa Misri huwa wanasaidiwa pia na uimara wa klabu zao kubwa za nyumbani.

Kwa sasa acha tuendelee kuishuhudia hii nuksi iliyopo. Nuksi ya kwamba Yanga akiwa juu lazima Simba awe chini, au Simba akiwa juu lazima Yanga awe chini. nimejaribu kuikutanisha Yanga ya miaka michache iliyopita na Simba hii nimejenga taswira kwamba ingekuwa mechi tamu na ya kusisimua zaidi katika ukanda huu.