Hawa wanasepa Man United Januari

Thursday December 6 2018

 

London, England. Wakati dirisha la usajili wa Januari likikaribia kufunguliwa, wachezaji watano wanaotarajiwa kuondoka Manchester United wamefahamika.

Wachezaji hao wanaojiandaa kuondoka Old Trafford ni pamoja na Marcos Rojo,  Eric Bailly, Phil Jones, Andreas Pereira pamoja na mkongwe Ashley Young, 34, ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu Juni mwakani.

Eric Bailly beki kutoka Ivory Coast, aliyenunuliwa kwa Pauni 30 milioni kutoka Villarreal ya Hispania, ameanza katika michezo mitano pekee kati ya 15 ambayo timu hiyo imecheza hadi sasa.  

Wachezaji hao wameongeza idadi ya wachezaji wasioiva na kocha wao Jose Mourinho, ambaye awali alikuwa akizozana vikali na Paul Pogba, Antonio Valencia na Alexis Sanchez.

Ingawa wachezaji hao ndio wanaoonekana wataihama Man United iwapo Mourinho ataendelea kuwepo Old Trafford, lakini kuna uwezekano kuwa hata Pogba na wengine wasiotarajiwa wanaweza kuondoka.

Mourinho amekaa kimya kuzungumzia juu ya uhusiano wake mbaya na wachezaji katika kinachoonekana anahofia hilo likijadiliwa na vyombo vya habari vya Uingereza linaweza kumuharibia kibarua chake.

Kocha huyo amekuwa akishutumiwa kutokana na matokeo duni inayoyapata Man United tangu alipoanza kuinoa mwaka 2016, tofauti na matarajio ya wamiliki.

Advertisement