#WC2018: Hazard mguu mmoja Chelsea, mwingine Real Madrid

Sunday July 15 2018

Kiungo wa Chelsea na timu ya taifa Ubelgiji,

Kiungo wa Chelsea na timu ya taifa Ubelgiji, Eden Hazard. 

Moscow, Russia. Baada ya kuisaidia Ubelgiji kumaliza katika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Dunia 2018, yanayomalizika rasmi leo, Kiungo wa Chelsea, Eden Hazard na Kipa wake Thibaut Courtois wameendelea kuwaruga mashabiki wa Chelsea kutokana na kauli zao tata, kuhusu hatma yao.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada yankukabidhiwa medali za mshindi wa tatu uwanjani St Petersburg, Hazard na Courtois kwa nyakati tofauti walionesha kutamani ufalme wa Real Madrid huku sehemu fulani ya moyo wao ukionesha kuwa na mapenzi na klabu yao ya sasa, Chelsea hasa baada ya ujio wa Kocha mpya, Maurizio Sarri.

Katika kauli yake iliyozua maswali mengi, Hazard anayewindwa na Real Madrid kama mbadala wa Cristiano Ronaldo aliyetimkia Juventus ya Italia, alinukuliwa akisema:

"Baada ya kuitumikia Chelsea kwa miaka sita ya mafanikio, huu unaweza ukawa muda mwafaka wa kujaribu mvinyo tofauti"

"Baada ya Kombe la Dunia, naweza kuamua hatma yangu, naweza kuamua niende wapi, naeza kuamua kwenda au kubaki, lakini ieleweke kwamba Chelsea ndio wenye maamuzi ya mwisho, wakitaka niende nitaenda ila wakiamua kunibakisha pia itakuwa sawa. Hata hivyo, ikitokea naondoka nadhani kila mtu anaelewa moyo wangu unapenda niende wapi."

 

 

Wakati Hazard akitoa kauli hiyo, Kipa wa Chelsea, Thibaut Courtois, naye alinukuliwa akisema: " Tumeshamaliza kazi iliyotuleta Russia, sasa nataka nikazungumze na wakala wangu kuhusu hatma yangu. Niko tayari kwa lolotez kubaki au kuondoka, japo natamani kubaki, lakini kama ni kuondoka nadhani kila mtu anaelewa."

"Mara nyingi watu huwa wanalalamika kuwa wachezaji hawaheshimu mikataba yao, sio kweli. Sidhani kama watamuweka benchi mtu mwenye uwezo mkubwa kama mimi, natamani kubaki kwa sababu naipenda London, ila ofa nzuri ikija..."

Courtois alisajili na Chelsea mwaka 2011, akapelekwa Atletico Madrid kwa mkopo na msimu wa 2015 akarejea klabuni. Kwa upande wake, Eden Hazard alitua Stamford bridge mwaka 2012.

Advertisement