Hesabu hizi kuibeba Serengeti Boys Afcon

Dar es Salaam. Ni miujiza inayoweza kuipeleka timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ katika hatua ya nusu fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) zinazoendelea nchini.

Baada ya kupoteza mchezo wa pili wa Kundi A juzi dhidi ya Uganda kwa kufungwa mabao 3-0, Serengeti Boys sasa inategemea hesabu zake ziwe sahihi katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya Angola ili iweze kutinga nusu fainali na kukata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Brazil, Oktoba, mwaka huu.

Serengeti Boys inayoshika mkia kwenye kundi lake ikiwa haina pointi, inapaswa kuhakikisha inaibuka na ushindi wa kuanzia mabao 4-0 dhidi ya Angola katika mchezo wa mwisho utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Jumamosi saa 10:00 jioni ili kufikisha pointi tatu.

Wakati huo itakuwa ikiombea Nigeria iibuke na ushindi wa kuanzia mabao 3-0 dhidi ya Uganda katika mchezo mwingine wa kundi hilo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex siku hiyo.

Ikiwa matokeo hayo yatatokea, maana yake Angola, Serengeti Boys na Uganda kila moja itakuwa na pointi tatu na hivyo kuruhusu kutumika kanuni zilizowekwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) za kuamua mshindi ikiwa timu zimelingana pointi.

Kigezo cha kwanza kinachoangaliwa ikiwa timu zimelingana pointi ni matokeo baina yao, ambacho hakitaweza kutumika kwa sababu hakuna atakayenufaika kwani Angola itakuwa imefungwa na Serengeti Boys ambayo nayo itakuwa imefungwa na Uganda iliyofungwa pia na Angola.

Kigezo hicho kitarukwa kwenda hadi cha pili ambacho ni utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa baina ya timu ambazo zimelingana pointi, ambacho kwa mantiki hiyo ndicho kitaibeba Serengeti Boys.

Uganda kufungwa mabao 3-0 na Nigeria maana yake itakuwa na tofauti ya mabao ya kufungwa na kufungwa -1 na ikiwa Serengeti Boys itapata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Angola maana yake utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa utakuwa 0 jambo litakaloipeleka nusu fainali kwa kuwa Angola itakuwa na -4.

Lakini timu hizo zikilingana kwa kigezo cha pili, bado Serengeti Boys itabebwa na kigezo cha tatu ambacho ni wingi wa mabao ya kufunga ambayo hadi sasa ina manne, Uganda matatu na Angola moja.

Akizungumza jana, Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema hawawezi kukata tamaa na watahakikisha wanapambana hadi hatua ya mwisho kuona kitakachotokea.

“Kimahesabu bado tuna nafasi jambo la msingi ni kuwajenga watoto kisaikolojia waamini kuwa bado wanaweza kufanya kitu na kisha kuombea Uganda wapoteze dhidi ya Nigeria.

“Mambo yamekwenda kinyume cha matarajio yetu kwa kupoteza mechi mbili za mwanzo lakini wakati mwingine mpira unakuwa hivyo.

“Wote tumeumizwa kwa matokeo haya na tunawaomba radhi Watanzania,” alisema Mirambo.