Hesabu zambeba Aussems ligi kuu

Muktasari:

  • Simba imevuna pointi tatu baada ya kuilaza Yanga katika Ligi Kuu

Dar es Salaam. Hesabu, uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja, uimara wa safu ya kiungo na mabadiliko ya kimbinu iliyofanya ndani ya uwanja, vimechangia ushindi wa bao 1-0 iliyopata Simba dhidi ya Yanga juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pamoja na safu ya ulinzi ya Yanga kucheza kwa nidhamu na kuwadhibiti vyema washambuliaji wa Simba katika sehemu kubwa ya mchezo huo, lakini bao la dakika ya 71 la Meddie Kagere lilitosha kuipa Simba pointi tatu.

Ni bao lililotokana na juhudi binafsi za nahodha John Bocco ambaye alifanya kazi ya ziada kumtoka Gadiel Michael na kupiga krosi iliyounganishwa vyema kwa kichwa na Kagere na kujaa wavuni.

Simba ilitawala sehemu kubwa ya mchezo ambapo wachezaji wake walipigiana idadi kubwa ya pasi, kumiliki mpira na kutengeneza nafasi jambo lililowalazimisha Yanga kurudi nyuma na kujilinda muda mrefu.

Ubora wa wachezaji mmoja mmoja wa Simba katika kumiliki mpira, kulivunja nguvu ya eneo la kiungo la Yanga ambalo lilijikuta likiachia mianya ambayo ingeweza kusababisha kuruhusu bao.

Na ndivyo ilivyotokea kwa bao la Simba ambalo ni zao la pasi iliyopigwa katika mwanya ulioachwa na mabeki wa Yanga na kumkuta Bocco aliyepiga krosi kwa Kagere aliyemuhadaa kipa Ramadhani Kabwili.

Lakini ujanja wa benchi la ufundi Simba kubadilika kwa haraka na kutumia mipira ya pembeni kujenga mashambulizi badala ya kupitia katikati kama ambavyo imekuwa ikifanya mara kwa mara, kulisaidia kuipa ufanisi ndani ya uwanja tofauti na wapinzani wao.

Awali, Simba ilianza kushambulia kupitia katikati mbinu ambayo ilidhibitiwa vyema na Yanga ambayo ilijaza idadi kubwa ya wachezaji eneo hilo na kufanikiwa kutibua mashambulizi ya Simba.

Hesabu za Simba zilifanya kazi vizuri zaidi baada ya kuingia kwa kiungo Hassan Dilunga aliyechukua nafasi ya Cletous Chama kuliimarisha timu hiyo ambapo iliongeza kasi ya kutengeneza nafasi zilizosababisha mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Yanga.

Wakati Simba ikifaidika kwa mabadiliko hayo ya kumuingiza Dilunga, Yanga iliangushwa na mabadiliko ya kuwatoa Amissi Tambwe na Ibrahim Ajibu na kuingia Mrisho Ngassa na Mohammed Issa ‘Banka’.

Ngassa aliyetegemewa kumfanya beki Zana Coulibaly asipande na kuleta madhara alishindwa kutimiza jukumu hilo sawa na Banka ambaye hakuongeza nguvu katika kiungo kama ilivyotarajiwa.

Kwa upande mwingine ulikuwa ni mchezo wa kihistoria kwa mabeki wa kulia Paul Godfrey ‘Boxer’ wa Yanga na Coulibaly upande wa Simba.

Godfrey aliyepandishwa na Yanga msimu huu akitokea kikosi cha vijana wenye umri chini ya miaka 20, alionyesha kiwango bora kwa kuwadhibiti vyema washambuliaji wa Simba na kusaidia kupandisha mashambulizi mara kwa mara kama ilivyokuwa kwa Coulibaly.

Kauli za wadau

Kocha wa Alliance, Kessy Mziray alisema Simba ilistahili kupata ushindi.

“Kwanza niwapongeze wachezaji wa Yanga kucheza vizuri hasa namba mbili. Kipindi cha pili nadhani kocha alipaswa kuendelea kuwaheshimu Simba kama alivyofanya cha kwanza. Simba nao walicheza vizuri, lakini walikuwa na matatizo mawili yaliyowagharimu ambayo ni kutokuwa na mipango mizuri kwenye eneo la ushambuliaji pamoja na uchoyo.

“Kingine nilichokibaini ni uwezo wa mchezaji mmoja mmoja Simba ndio maana mabadiliko yao yalibadilisha timu tofauti na Yanga ambayo mabadiliko waliyofanya yaliwagharimu,” alisema Mziray.

Kocha msaidizi wa Namungo FC ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga na Simba, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ alisema kilicholeta utofauti ni ubora wa nyota wa kigeni hasa Meddie Kagere.

“Ukiangalia Yanga walifanikiwa kuwadhibiti Simba na hakukuwa na tofauti kubwa ndani ya uwanja, lakini mwisho wa siku Kagere alitumia uwezo binafsi kuunganisha haraka mpira wa krosi ya Bocco na kuupeleka eneo ambalo Kabwili asingeweza kuokoa.

Katika hatua nyingine, Ligi Kuu iliendelea jana ambapo Lipuli ililazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Singida United, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Samora mkoani Iringa.