Hofu ya Mkude corona yawagusa makocha Ligi Kuu

Dar es Salaam. Kauli ya kiungo wa Simba, Jonas Mkude kuwa endapo Ligi Kuu Bara itaendelea baada ya muda wa kusimama, kutakuwa na changamoto mbalimbali kwa wachezaji kurejea kwenye ari ya mchezo ikiwamo suala la kukosa pumzi na majeraha, imewaibua makocha ambao wamemuunga mkono.

Mkude alisema juzi kuwa changamoto kubwa anayoiona iwapo wachezaji watarejea ni kwamba wengi wao watakabiliwa na suala la uwiano tofauti wa pumzi ikiwamo baadhi yao kukata mapema, jambo ambalo litaziathiri timu nyingi katika juhudi za kusaka ushindi.

Mchezaji huyo alienda mbali zaidi akasema kutokana na kila mtu kufanya mazoezi kivyake haamini kama kila mmoja anajibidisha kuyafanya ipasavyo huko aliko kwa sasa.

Ligi mbalimbali za soka duniani zimesimama kupisha juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa corona ambao umekuwa changamoto na kusababisha mambo mengi kusimama.

Wanachosema makocha

Kauli hiyo ya Mkude imewaibua baadhi ya makocha ambao wamesema licha ya changamoto zinazowakabili wachezaji kwa sasa, tatizo ni tabia zao.

Kocha wa Gwambina FC, Athuman Bilali ‘Bilo’ alisema wanawatambua wachezaji wao hivyo pamoja na kuwapa programu za kufanya kwa ajili ya kujiweka fiti, bado watakuwa na kazi ya kufanya ligi itakapoanza.

Alisema jukumu kubwa ambalo wataanza nalo watakaporudi kwenye majukumu yao ni kutafuta pumzi kwa wachezaji na kuwa fiti kwa ajili ya mechi (match fitness) ili kuwarudisha michezoni kutokana na kufanya mazoezi magumu bila ya kucheza mchezo wowote.

“Wachezaji sio wote ambao wanaweza kufuata programu walizopewa, kuna wanaojitambua watafanya hivyo na wengine watabweteka, hivyo ni ngumu kuwakuta wakiwa kwenye usawa. Ni jukumu letu kama makocha kuhakikisha tunawaweka sawa,” alisema.
Kocha msaidizi wa timu ya Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, Joseph Lazaro alisema uvivu walionao baadhi ya wachezaji hapa nchini kujituma kufanya mazoezi ni kazi kubwa.

Alisema kutokana na mapumziko waliyopewa, itakuwa kazi kubwa kwa makocha pale watakaporejea kutoka majumbani kwao.

Lazaro alisema kujituma kwa wachezaji ni vigumu na ni wachache wanaoweza kufanya mazoezi ya nguvu.

“Wachezaji kujituma wenyewe bila msukumo wa mwalimu ni shida, tunawajua na hapa watakaporejea sijui itakuwaje ngoja tuone,” alisema.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kenny Mwaisabula alisema kazi kubwa itakuwa kwa wachezaji wa ndani huku akisisitiza kuwa ndio wasiojitambua hivyo watatakiwa kuandaliwa upya na sio kuwategemea kwa programu walizoachiwa.

Alisema ameshuhudia wachezaji wengi wakifanya mazoezi gym na wengine michangani kwa lengo la kutafuta pumzi lakini hana uhakika kama wanafanya kama inavyotakiwa.

“Wachezaji nina hakika watarudi wakiwa wamechosha miili yao kwa kufanya mazoezi ya nguvu na watakuwa hawajaambulia chochote zaidi watawapa kazi makocha wao kuanza kuwatafutia mechi fitness,” alisema.

Mwaisabula aliongeza kuwa mazoezi wanayofanya hayana ushindani kama inavyokuwa maandalizi ya msimu ambapo kunakuwa na mipira maalumu kwaajili ya wachezaji kucheza na kukimbia huku kukiwa na sambamba na mazoezi ya viungo kitu ambacho sasa hakifanyiki.

Msisitizo wa Mkude

Akizungumza na Mwananchi, Mkude alisema kila mchezaji anafanya mazoezi kivyake na kuna wanaofanya mara tatu, mbili na wengine mara moja huku kila mtu akifanya kwa muda autakao hivyo itakuwa ngumu kupata kikosi kilicho na uwiano mzuri.

“Mazoezi ya kujitenga kila mmoja yana manufaa kwa kila mchezaji, kwa timu sina hakika kwenye hilo kwani ugumu ni pale tutakapokutana na kila mmoja kuwa na pumzi tofauti maana kutakuwa na waliokuwa wanajituma sana na waliokuwa wanategea,” alisema.

“Kikubwa ninachoweza kusema tutakutana na ugumu na itakuwa ni changamoto kwetu kwani tumeachana tukiwa tumetoka katika muunganiko mzuri na tupo fiti kwa upambanaji sidhani kama tutarudi hivyo,” alisema.

Mkude aliongeza kuwa imani yake kila mchezaji aliyepo nyumbani anajitambua na anatambua kuwa kuna ligi bado itaendelea hivyo alitumia nafasi hiyo kuwashauri kufanya mazoezi kwa wakati ili wakirudi waendeleze kasi na kufikia malengo.

Simba ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara na inaongoza kwa pointi ikiwa ya kwanza kwenye msimamo baada ya kujikusanyia pointi 71.

(Nyongeza na Clezencia Tryphone).