IAAF yaiongezea kibano Russia hadi 2019

Wednesday December 5 2018

Zurich, Uswisi. Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Riadha (IAAF), Lord Sebastian Coe, amesema wameiongezea adhabu ya Russia kwa wanariadha wake kutoshiriki mashindano yoyote ya kimataifa hadi mwaka 2019.

Coe alisema kuwa IAAF ilitaka ipewe sampuli ya vipimo kutoka wakala wa kupiga vita matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni (Wada) kutoka Russia lakini nchi hiyo haikutekeleza.

Alisema kutokana na muda waliotoa kwa nchi hiyo  kuwasilisha sampuli hizo kumalizika licha ya kuwakumbusha mara kadhaa wameona ni vyema adhabu iendelee.

“Kitendo cha kutopewa ushirikiano na mamlaka mjini Moscow, kimetufanya tuamini kile tulichokuwa na wasiwasi nacho tangu mwanzo kwamba serikali ya Russia ilihusika na suala hili,” alisema Coe.

Kutokana na uamuzi huo Russia ambayo wanariadha wake hawajashiriki mashindano yoyote ya kimataifa tangu mwaka 2016 wataendelea kuyakosa mashindano yote.

Bodi ya Olimpiki iliifungia Russia kushiriki mashindano yote ya kimataifa Novemba 2015 baada ya kubainika kuwa serikali ilihusika kuwapa wanariadha wake dawa maalumu  za kuongeza nguvu ili waweze kutamba kimataifa.

Hata hivyo adhabu hiyo inaweza kuendelezwa iwapo Moscow, hawatawasilisha sampuli za vipimo zitakazothibitishwa na maabara nyingine kuwa hivi sasa hakuna anayetumia dawa hizo.

Aidha Russia imeamriwa kulipa gharama zote zitakazohusu maofisa wa IAAF, wakati wa ufuatiliaji, upimaji na uchunguzi wa sampuli za wanariadha wake hadi ukweli utakapobainika.

“Tunaamini Russia watawasilisha sampuli na data zote kuhusiana na kadhia hii, kufikia mwishoni mwa mwaka huu," alisema Rune Andersen mkuu wa kitengo cha kufuatilia sakata hilo.

Alisema tarehe ya mwisho kwa Russia kuwasilisha uthibitisho huo wa sampuli ni Desemba 31 lakini wakishindwa kutekeleza wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kurefushwa kwa muda wa kifungo chao.

Uamuzi huo umekuja baada ya IAAF kutupa rufaa ya tisa iliyowasilishwa na Russia kupinga wanariadha wake kuzuiwa kushiriki mashindano yote ya kimataifa.

Kufungiwa kwa wanariadha wa Russia kulisababisha pia Kamati ya kimataifa ya Olimpiki (IOC), kuiengua nchi hiyo katika mashindano yake yakiwemo yale ya Olimpiki ya kipindi cha baridi yaliyofanyika Korea Kusini, mwaka huu ‘2018 Pyeongchang Winter Games’.

Ni mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 70, wanariadha wa Russia mwaka huu hawakuruhusiwa kuiwakilisha nchi yao katika mashindano ya ubingwa wa Ulaya.

Wanariadha hao waliruhusiwa kushiriki kama washiriki binafsi, hivyo hawakupeperusha bendera ya nchi yao wala kupigwa wimbo wa Taifa pale waliposhinda.

Katika hatua nyingine IAAF imetangaza kuwa ubingwa wa Dunia wa riadha kwa mwaka 2023 utafanyika mjini Budapest, nchini Hungary.

Advertisement