Imelda Marcos matatani kwa rushwa

Friday November 9 2018

Manila, Ufilipino. Mahakama Kuu imemtia hatiani Imelda Marcos na imeamuru akamatwe katika hukumu nadra kutolewa dhidi ya mwanamama huyo aliyeshutumiwa pamoja na mumewe dikteta wa zamani Ferdinand Marcos, kwa rushwa na ubadhirifu wa mabilioni ya dola mali ya Serikali.
Hata hivyo, Marcos mwenye umri wa miaka 89 anaweza kukata rufaa ambayo itamruhusu aendelee kuwa huru wakati kesi inanguruma katika nchi ambayo mfumo wa sheria unasifika kwa ubaya.
Hukumu kutoka mahakama ya kupambana na rushwa ya Sandiganbayan inamtaka mama huyo kutumikia kifungo cha chini cha miaka sita kutokana na mashtaka kwamba wawili hao walifyonza kiasi cha dola 200 milioni kupitia taasisi za Uswisi miongo iliyopita.
Ferdinand Marcos, ambaye pamoja na mkewe walishutumiwa kudokoa dola 10 bilioni za walipakodi wa Ufilipino, alitorokea Marekani baada ya kuibuka machafuko yaliyokomesha utawala wake wa miaka 20 mwaka 1986.
Marcos alifariki dunia mwaka 1989 akiwa uhamishoni ingawa familia yake ilirudi Manila na tangu hapo wakarejea kwenye siasa. Imelda Marcos kwa sasa ni mbunge.

Advertisement