Ishu ya Yanga na Ndemla iko hivi

KUMEKUWA na taarifa nyingi mtaani zikimuhusisha kiungo wa Simba, Said Ndemla na Yanga hasa kutokana na nafasi yake kucheza ndani ya kikosi cha kwanza kuonekana ni finyu huku mkataba wake pia ukielekea ukingoni.

Timu ambayo amekuwa akihusishwa nayo zaidi ni Yanga ambayo inatajwa baadhi ya viongozi wameshamcheki kwenye simu.

Ndemla amezungumza na Mwanaspoti na kufafanua mambo kadhaa ikiwemo hatma yake ya msimu ujao anaweza kufanya maamuzi gani.

KUHUSU YANGA

Amesisitiza kuna mambo mengi amekuwa akiyasikia mitaani yakimhusisha na Yanga lakini si rasmi. Bado ni mali ya Simba kutokana mkataba wake bado haujamalizika.

Ndemla anasema mara baada ya msimu kumalizika mkataba wake ndio utakuwa unafikia ukingoni na mpaka sasa msimu bado haujamalizika kwani wamebakisha mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na kombe la Shirikisho (FA).

“Nadhani baada ya kumaliza mechi za mashindano hayo yote mawili ndio msimu utakuwa umemalizika na mkataba wangu utakuwa umeisha ndani ya Simba na hapo ndio naweza kueleza hatma yangu,” anasema.

“Kuhusu Yanga kunitaka au timu nyingine yoyote hilo linatokea kwa mchezaji yoyote mzuri lakini halitakuwa jambo jema kuanza kuzungumza masuala haya wakati bado natakiwa kutoa mchango wangu katika timu yangu ya Simba ili kufikia mafanikio ya kufanya vizuri kwenye ligi na FA,” anasema Ndemla.

“Nimekuwa nikiziona na kusikia taarifa hizo za kujiunga na Yanga lakini ukweli akili na nguvu yangu ipo katika kikosi cha Simba kwani bado tunakazi kubwa ambayo hatujaimaliza katika msimu huu,” anasema.

MAISHA YA SIMBA

Tangu ameanza kucheza katika kikosi cha Simba si chini ya miaka kumi lakini Ndemla ameshindwa kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza kwa makocha tofauti.

Ndemla anasema kwa muda wote aliokuwa katika kikosi cha Simba amekuwa mchezaji wa kupambana na kutamani kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine kuna muda ambao anafanikiwa lakini wakati mwengine inakuwa tofauti.

“Kama mchezaji jukumu langu la kwanza ni kutamani kutoa mchango katika timu yangu haswa kucheza katika kikosi cha kwanza mara kwa mara sasa jambo hilo linaposhindikana huwa najisikia vibaya,” anasema.

“Kama umenifuatilia kwa karibu kuna baadhi ya makocha wamekuwa wakinitumia katika kikosi cha kwanza lakini kuna wengine limeshindikana hilo kwangu nalichukulia kama changamoto na naendelea kulifanyia kazi,” anasema.

KUCHEZA NJE

Katika vipindi tofauti Ndemla amekuwa akienda kufanya majaribio katika timu mbalimbali nje ya Tanzania haswa katika nchi ya Sweden, kuna wakati zilitoka taarifa amefuzu na anakwenda kucheza soka la kulipwa huko lakini baada ya muda tunaendelea kumwona tena hapa nchini.

“Kwangu naimani wakati tu ulikuwa haujafika ila ukifika nitaenda kucheza soka la kulipwa huko nje ya Tanzania kwani moja ya malengo ambayo yapo katika maisha yangu ya soka ni hilo,” anasema Ndemla.

AENDE WAPI?

Baadhi ya mashabiki na wapenzi mbalimbali wa soka hapa nchini wamekuwa wakijiuliza kwa nini Ndemla anashindwa kuondokana na kwenda kutafuta changamoto katika timu nyingine kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara.

“Nimekuwa nikifuatilia na kuangalia watu mbalimbali wakinizungumzia niondoke hapa Simba niende katika timu nyingine kutokana na kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara sasa jambo rahisi la kujiuliza natoka hapa nakwenda wapi bila ya kuwepo mpango maalum huko ambapo nakwenda,” anasema.

“Lazima nifahamu malengo na hatma yangu huko na nakwenda kucheza mpira kwa maana timu nyingine ambayo watu wengi wanazungumza niende nisije kukutana na mazingira magumu zaidi ya hapo na nacheza sasa.

“Lakini mbali ya maneno yote hayo ambayo yamekuwa yakizungumzwa mimi ndio natambua hatma ya maisha yangu ya hapo baadae baada ya mpira kwa maana hiyo hata haya maamuzi yangu naomba yaendelee kuheshimiwa,” anasema Ndemla.

USHINDANI

Katika kikosi cha Simba kumekuwa na ushindani wa namba si msimu huu tu bali katika misimu yote ambayo Ndemla amecheza na huenda jambo

hilo limechangia kwake kushindwa kuwa katika kikosi cha kwanza mbali ya uwezo aliokuwa nao. Ndemla alisema hakuna timu ambayo haina ushindani wa namba jambo hilo basi lipo pia katika kikosi cha Simba lakini anaendelea kupambana kadri ambavyo anaweza ili aweze kulishinda na kupata nafasi ya kucheza.

“Ni kweli ushindani ni mkubwa haswa katika eneo la kiungo ambalo nacheza mimi lakini mapambano bado yanaendelea naimani nitapata nafasi ya kucheza bado sijakata tamaa katika hilo,” anasema Ndemla.