JICHO LA MWEWE: Tshishimbi mfanyabiashara mzuri wa saini yake

NILIMUONA Pappy Tshishimbi majuzi akiongea na redio mbili katika nyakati tofauti. Redio ya kwanza aliongea nayo kwa njia ya simu. akajinadi kwamba yuko sokoni na mkataba wake unakaribia kumalizika. Nilitabasamu.

Redio nyingine akaenda studio kabisa. Akaongea kuhusu lile lile suala la mkataba wake. inaonekana viongozi wa Yanga walikuwa wamechukia kutokana na kitendo cha kuzurura katika vyombo vya habari. Nilicheka zaidi.

Kwa akili ya kawaida ziara ya Tshishimbi haikuwa ya bahati mbaya. Ilikuja katika wakati ambapo mabosi wa Yanga walikuwa wameingia katika mgogoro na kampuni ya GSM ambayo kwa sasa inaidhamini na kuifadhili Yanga kwa wakati mmoja.

Tshishimbi, kama ilivyo kwa Ben Morrison na Haruna Niyonzima ni mastaa ambao wana uhusiano mzuri na kampuni ya GSM. Si ajabu aligeuzwa kuwa ‘ujumbe’ kwa viongozi wa Yanga kutoka kwa GSM kwamba ‘Muongezeeni mkataba sisi tumejitoa’.

Kwanini aongelee wakati huu kwa mkataba unaomalizika mwezi Agosti? Baada ya Morisson kusaini mkataba mpya chini ya GSM, kisha GSM wakakorofishwa, nadhani kulikuwa na hali ya kupima upepo kutoka kwa GSM kwamba sasa suala la kumuongezea mkataba mpya Tshishimbi wanalo viongozi wa Yanga.

Na kama tunavyoelewa, kwa hali ilivyo pale Yanga, bila ya uwepo wa GSM suala la kumuongezea mkataba mpya Tshishimbi linaweza kuwa ‘maji marefu’ kwa viongozi waliopo. Haishangazi kuona haraka haraka Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla alichukua hatua dhidi ya viongozi wenzake wanaoikorofisha GSM.

Na hapo hapo GSM wakarudi katika shughuli zao za kawaida za kuikagharamia Yanga nje ya masuala ya mkataba. Muda si mrefu watamalizana na Tshishimbi kama ilivyokuwa kwa Morisson. Hii ndio hali halisi ya kilichoendelea katika ziara ya Tshishimbi kwa vyombo vya habari.

Lakini tuachane na hisia hizi. Ukweli ni kwamba Tshishimbi amefanya kazi nzuri ya kujinadi mitandaoni. Mchezaji hakatazwi kuelezea suala lake la mkataba pindi mkataba wenyewe unapotiririka kuelekea mwishoni. Inawezekana kosa kubwa lilikuwa kuongea na vyombo vya habari bila ya ruhusa ya mwajiri wake lakini kusema kwamba yupo huru hakukuwa na kosa lolote.

Tatizo lingekuja kama bado angekuwa na mkataba wa miaka miwili pale Yanga. Yanga wangehoji ni namna gani anaweza kuongea na waandishi wa habari kuhusu mkataba wake huku akiwa na mkataba wa muda mrefu klabuni.

Lakini hapo hapo Tshishimbi anatufundisha jambo. Kwa kipindi ambacho ameichezea Yanga ameifanya kazi yake vema. Ni mmoja kati ya wachezaji watatu muhimu klabuni. Amejiweka katika nafasi nzuri ya kuzigonganisha kichwa klabu kubwa nchini, Yanga, Simba na Azam.

Mwenyewe anajua kwamba kuna watu wa Simba wanampenda, wanamkubali na wanamtaka. Anajua kwamba huu ni wakati wake wa kuziingiza timu mnadani. Inawezekana hapo katikati kiwango chake kiliyumba lakini kuelekea mwishoni mwa msimu huu kiwango chake kinamuweka sokoni vizuri.

Kupiga kelele kwamba mkataba wake ulikuwa unafika mwisho ilikuwa ni njia nzuri ya kujinadi. Kupiga kelele namna anavyowapenda baadhi ya wachezaji wa Simba ilikuwa meseji tosha kwa watu wa Yanga na watu wa Simba.

Kwa watu wa Yanga alikuwa anamaamisha kwamba anaweza kucheza Simba kama ikimuhitaji na hana tatizo na watu wa Simba. Kwa watu wa Simba alikuwa anawakaribisha mezani ili wafanye naye mazungumzo kama wakitaka kumuunganisha na viungo wa Simba.

Wachezaji wetu wazawa wana tatizo moja. Wanacheza katika klabu hizi wakijiona kama Wanachama. Kwa mfano, wakati mkataba wa Ibrahim Ajibu ukielekea mwisho pale Jangwani hakuonekana kujiweka sokoni kwa watu wa Yanga ili Simba wapande dau zaidi.

Alionekana kupeleka kichwa chake Simba moja kwa moja huku pia akifanya ujinga mwingine wa kuikataa TP Mazembe hadharani. Simba hawakuwa na upinzani katika kuinasa saini yake. Ajibu alipaswa kuwa mfanyabiashara mzuri kuelekea mwisho wa mkataba wake Yanga.

Wakati akitoka Yanga kwenda Simba, Haruna Niyonzima alifanikiwa kuzitingisha timu zote mbili. Alitengeneza mazingira ya kutojulikana wapi alikokuwa amepania kwenda. Mwishowe aliishia kwenda Simba kwa dau kubwa.

Tatizo jingine la wachezaji wetu ambalo wanapaswa kumuiga Tshishimbi ni kuhakikishia kwamba wanakuwa watamu wakati wakielekea mwisho wa mikataba yao. Hivi Said Ndemla akikaribia kufika mwisho wa mkataba wake anaweza kuiweka Simba roho juu? Vipi kwa Fey Toto? Vipi kwa Abdulaziz Makame? Sidhani.

Huyu Mcongo amefanya kazi kubwa ya kuhakikisha kwamba anaendelea kuwa kiungo namba moja wa Yanga. Anapiga kazi kweli kweli. Ameletewa Fey, Makame, Mohamed Banka na wengineo ambao walionekana kama vile wangeweza kumfunika kutokana na vipaji vyao maridhawa lakini Tshishimbi ameendelea kuwa muhimu kwa sababu anajituma zaidi.

Hii ni namna sahihi zaidi ya kuwa mfanyabiashara wa saini yake mwisho wa mkataba. Hakuna njia nyingine zaidi.