JICHO LA MWEWE: Deo Kanda niliyewahi kumfahamu vema zamani

TAKRIBAN miaka 10 iliyopita nilikuwa jukwaa la mashabiki wa Simba. Uwanja mpya wa Taifa. Mechi ilikuwa ni kati ya Taifa Stars na DR Congo. Pambano la kirafiki. Hata hivyo, mchezaji anayeitwa Deo Kanda hakuwa na urafiki na mtu.

Alikuwa winga wa kushoto. Mtu aliyekuwa anakabana naye alikuwa Shadrack Nsajigwa Mwandemele. Nilicheka sana. Nsajigwa alikumbana na wakati mgumu kutoka kwa Kanda. Huyu Kanda alikuwa Kanda haswa. Alikuwa mwepesi aliyepitiliza.

Angeweza kudanganya kama anakwenda kushoto lakini ghafl angeghairi na kwenda kulia. Angeweza kudanganya kama anapiga, lakini ghafla angeghairi. Alikuwa msumbufu aliyepitiliza. Mashabiki wa Simba walikuwa wanafurahia wanachokiona. Nsajigwa alikuwa mchezaji wa Yanga. Mateso yake kwao yalikuwa furaha.

Wakati wa mapumziko kocha akamuingiza Said Nassoro ‘Chollo’ ambaye alikuwa beki wa Simba nyakati hizo. Kanda alizidisha mateso zaidi kwa Chollo. Safari hii mashabiki wa Simba walikaa kimya kama wamemwagiwa maji. Mpira wetu bwana.

Tangu siku hiyo nikawa napenda kulisikia jina la Deo Kanda. Sikuwahi kumsahau jinsi alivyowafurahisha na kuwanunisha mashabiki wa Simba. Maisha yanakwenda kasi zaidi ya kasi yenyewe.

Majuzi nikasikia Deo Kanda amesajiliwa Simba. Nikajiuliza, Deo Kanda huyuhuyu? Nikaenda kupekua kwa sasa ana umri wa miaka mingapi. Nikaona ana miaka 29. Kama ni takribani miaka 10 iliyopita inamaanisha Kanda aliyekuwa anafanya mambo yale wakati ule alikuwa na umri wa miaka 19? Nikaguna.

Ina maana Kanda alikuwa katika ukomavu ule akiwa na miaka 19 tu? Hapana. Haiwezekani. Wachezaji wa Afrika tunajuana wenyewe tu. Tuna siri yetu. Tuna mambo yetu. Tuna tamaduni zetu linapofikia suala la umri wa pasipoti na umri halisi.

Hapohapo nikawaza, inakuwaje Deo Kanda ambaye nilimfahamu, leo timu yake ya zamani TP Mazembe haimuhitaji tena? Vipi kuhusu AS Vita na wengineo? Wacongo wanalipa kuliko sisi, inawezekana Simba imetangaza dau kubwa kuliko Mazembe? Sidhani.

Swali jingine la kipuuzi nikajiuliza. Yule Deo Kanda ambaye nilimfahamu inakuwaje hakuwepo Misri na kikosi cha DR Congo? Enzi zake alikuwa mmoja kati ya wachezaji tishio katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Congo. Leo wakati wenzake wakiwa Cairo yeye alikuwa akitua Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Kambarage Nyerere.

Ni wazi Kanda hawezi kuwa Kanda yule yule. Alitesa zama za kina Nsajigwa na leo Nsajigwa tumemsahau, lakini yeye bado yupo tu. Hata kama anajitunza lakini hawezi kuwa yuleyule. Kuna sehemu amekwama, kama ambavyo timu iliyomchukua ilivyokwama.

Pamoja na kwamba nina hofu na kiwango cha Deo Kanda wa sasa, lakini inawezekana akatua nchini, akafanya makubwa, akaonekana mchezaji mpya. Ndivyo mpira wetu ulivyo. Unapokea makombo lakini yanaonekana kama chakula cha jana.

Kanda anaweza kuja na kusumbua mabeki wa wa pembeni wa Ligi Kuu katika kiwango ambacho wengine watakiona kama kile ambacho mimi nilikiona wakati anamsumbua Nsajigwa Shadrack, kumbe ni mchezaji wa zamani ambaye amepitwa na wakati kwao Congo na kwingineko kule wanakofahamu mpira.

Kilichonichekesha ni pale gazeti moja lilipoandika ‘Mrithi wa Okwi atua’. Kwamba Kanda amekuja kumrithi Emmanuel Okwi. Kwamba mchezaji wa umri wa Kanda amekuja kumrithi mchezaji mwenye umri wa Okwi. Nikaguna kidogo. Hata kama wote wamedanganya miaka lakini Okwi ana miaka 26 na Kanda ana miaka 29.

Hapohapo unafikiria jinsi ambavyo Okwi amesumbua katika fainali za Afcon pale Misri. Inakuwaje Simba inamtafuta mrithi wa Okwi kwa kumchukua mtu ambaye ameshindwa hata kwenda Cairo na kikosi chake cha timu ya taifa? Au tofauti ya viwango vya timu zao za taifa?

Kwa Simba nina ujumbe mmoja. Mambo mengi kuhusu usajili wao nitajaribu kuandika kesho au siku nyingine zijazo lakini usajili wa mchezaji kama Deo Kanda unaonyesha kusuasua kwa uwekezaji wa mastaa ndani ya kikosi chao.

Kila siku unasikia wapinzani wao ambako Simba wanataka kukaa anga hizo kina AS Vita, Al Ahly, AJ Saoura, Esperence, Raja Casablanca na wengineo wananunua wachezaji wa bei ghali kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao. Simba inamchukua mchezaji kama Kanda kwa sababu bado ana uzuri fulani na bajeti yao ndogo imewaruhusu.

Ningetamani imchukue mchezaji kama Kanda, lakini wa miaka 10 iliyopita. Nadhani mwekezaji hayupo tayari kutoa Dola 200,000 kwa ajili ya mchezaji mmoja. Lakini mchezaji kama Kanda wa miaka 10 iliyopita yupo sehemu akisubiri ofa hiyo.

Nadhani bado tupo katika bei za kina Ibrahim Ajibu, hasa wanapokuwa wachezaji huru.

Kama tunajidanganya kwamba kila kitu kitakwenda kama msimu uliopita ulivyokwenda nadhani haitakuwa sawa.

Kila msimu una changamoto zake ndani na nje ya uwanja. Tatizo naona kuna kuridhika kwa kiasi kikubwa kwa mashabiki na viongozi wa Simba ambao wengi wao wanaamini kwamba timu yao itaanzia pale ilipoishia msimu uliopita. Sio kitu rahisi sana kitu kama hicho