Jahazi la Genk ya Samatta lazidi kuzama Ubelgiji

Muktasari:

KRC Genk imetupwa nje ya kombe la FA Ubelgiji baada ya kukumbana na kipigo cha penalti 4-3 huku Samatta akifunga moja, baada ya dakika 120 ya mchezo huo kumalizika kwa sare ya mabao 3-3.

Dar es Salaam. Jahazi la KRC Genk ya Mbwana Samatta limezidi kuzama baada ya kuondolewa katika robo fainali ya Kombe la FA Ubelgiji kwa kufungwa kwa penalti 4-3 na Antwerp.

Genk haina matokeo mazuri katika Ligi Kuu Ubelgiji, imepoteza nafasi nyingine ya kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kukubali kulazimishwa sare 2-2 katika dakika 90 za mchezo war obo fainali hivyo zikaongozwa dakika 30 ambazo na zenyewe zilishindwa kutoa mbabe.

Katika dakika 30 za nyongeza, Antwerp waliitangulia Genk kwa kuifunga bao dakika ya 104 kupitia kwa Dieumerci Mbokani, lakini Genk ilisawazisha dakika ya 105 kupitia kwa Junya Ito.

Samatta aliyecheza kwa dakika zote 120, hakufunga bao hadi katika hatua ya mikwaju ya penalti ambapo aliifungia penalti ya kwanza.

Licha ya Samatta kufunga mkwaju huo, KRC Genk ilijikuta ikipoteza mchezo baada ya Ito na Wouters kupoteza mikwaju yao ya penalti huku wapinzani wao wakifunga.

Matokeo hayo, yameifanya KRC Genk kuendelea kuvurunda katika michezo yao ya mashindano mbalimbali, tangu kutimuliwa kwa Felice Mazzu, wakiwa chini ya Hannes Wolf wameshindwa kuibuka na ushindi katika mchezo hata mmoja.