Jicho la Mwewe: Guardiola anazidi kuliacha soka la Bongo gizani

Muktasari:

  • Ugunduzi huu wa Pep umenitafakarisha jinsi ambavyo tuko mbali na dunia ya wenzetu. Wakati sisi tukiwa na makipa au wachezaji ambao wanapata wakati mgumu na mambo ya msingi, akina Pep wanahama na kwenda dunia nyingine.

JANA nilikuwa nawaza kabla ya mechi ya Liverpool na Manchester City kuanza pale Anfield. Nikawaza jinsi ambavyo Pep Guardioala atakavyoichezesha timu yake. Nikawaza jinsi ambavyo Jurgen Klopp atakavyoichezesha timu yake.
Kwanza nikahofia namna ambavyo Guardiola angepata pigo kubwa langoni. Kipa wake namba moja Ederson aliumia katika pambano kati ya Man City dhidi ya Atalanta katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.
Unajiuliza, pigo kubwa zaidi la Guardiola kwa Ederson ni lipi? Amini usimiani, sio mikono yake. Ndio, Ederson anajua kuokoa michomo. Lakini Guardiola anaitegemea zaidi miguu ya Ederson kuliko mikono yake.
Kivipi? Guardiola anataka kipa wake awe mzuri katika kucheza mpira kwa miguu. Hataki kipa abutue. Anataka kipa aanzishe mpira kwa miguu kwa walinzi wake au viungo wake, ikiwezekana arudishiwe, awekwe katika presha na kisha kupitisha pasi nyingine kwenda kwa wachezaji wake. Hakuna kubutua.
Guardiola anaamini kwamba mpira unafika haraka zaidi ukitokea nyuma kama kipa habutui. Iwe ‘goal kick’ au vinginevyo. Bahati mbaya au nzuri, makocha wengine wote wameanza kumuiga. Karibu Ulaya nzima inataka kumuiga Pep.
Makocha wa Kiingereza wanalalamika kwamba Pep anataka kuvuruga mpira wao. Sam Allardayce ni miongoni mwa makocha wanaochukizwa na staili ya Pep. Ukikumbuka enzi zake alipenda kipa wake apige mpira mbele kwa ajili ya Kevin Nolan kugombania.
Ugunduzi huu wa Pep umenitafakarisha jinsi ambavyo tuko mbali na dunia ya wenzetu. Wakati sisi tukiwa na makipa au wachezaji ambao wanapata wakati mgumu na mambo ya msingi, akina Pep wanahama na kwenda dunia nyingine. Wanatupeleka wapi?
Kwanza kabisa kuwafikia akina Pep ni ngumu. Nikitazama kwa makipa wa ndani, ni Juma Kaseja tu ndiye ambaye anaweza kumuelewa Guardiola. Juma ndiye ambaye hana hofu na anaweza kucheza kwa kuanzia nyuma.
Hii ni siri kubwa kwanini kocha wa Taifa Stars hamtamani sana Aishi Manula na badala yake anampenda Juma. Etienne Ndayiragije anafuata mfumo wa akina Guardiola. Nguvu yake kubwa ni umiliki wa mpira, hasa kwa kuanzia nyuma.
Makipa wetu wengi kwa sasa wanasumbuliwa na matatizo ya msingi ya kazi yao. Wengine hawana ‘timing’ ya krosi au kona. Wengine ni dhaifu katika kujipanga kwa ujumla. Wengine ni dhaifu tu katika mashuti ya mbali. Vipi hili la akina Guardiola wataliweza?
Ina maana kwa sasa inabidi tuwafundishe makipa wetu jinsi ya kudaka, jinsi ya kuwa na ‘timing’. Halafu bado tunadaiwa na dunia ya kisasa kuwafundisha jinsi ya kucheza mpira kwa miguu. Ni kitu ambacho lazima tukubali kwa sababu dunia ya akina Guardiola inatuelekeza hilo.
Baada ya udhaifu wa makipa wenyewe tunakuja katika tatizo la pili. Viwanja vyenyewe viko wapi kwa makipa kucheza kutokea nyuma? Hakuna. Kuna viwanja vitano tu Tanzania nzima ambavyo vinaweza kumfanya kipa anayefikiria kuwa Ederson kufanya hivyo.
Uwa-nja wa Taifa, Uwanja wa Uhuru, Cha-mazi, Kaitaba na Nyam-agana. Kasoro uwanja mpya wa Taifa, viwanja vingine vyote ni vya nyasi bandia. Nadhani katika viwanja kama vya Mkwakwani, Nangwanda Sijaona, Namfua Singida, Majimaji Songea na vinginevyo vyote Guardiola angemuagiza Ederson abutue.
Hata huyu Kaseja ataleta mbwembwe za kupiga pasi kuanzia nyuma akicheza katika Uwanja wa Taifa tu. Akienda Mkwakwani hakuna anachoweza kufanya. Anaweza kupiga pasi murua kwenda kwa beki wake lakini mpira ukadunda katika tuta na kugeuza mwelekeo kwenda kwa adui.
Kitu kingine ambacho Pep na akina Klopp wamejaribu kukigundua ni ukabaji wa pamoja wa wachezaji wote katika staili ya kukaba kuanzia juu. Inaitwa ‘pressing’. Staili hii inaweza kutumika popote hapa Tanzania bila ya kujali uwanjani.
Klopp na Guardiola wanapenda wachezaji wao wakabe kwa kuanzia juu kule kule kwa mabeki. Binafsi naamini kwamba kama ningekuwa kocha ningewaambia wachezaji wangu watumie staili hii kwa muda mrefu tu. Kwanza ni kwa sababu viwanja vyetu ni vibovu kwa hiyo walinzi wanapoanziwa mpira wanakuwa hawana raha ya kuukokota vyema.
Kitu ambacho makocha wetu watashindwa ni ukweli kwamba ni vigumu kwa wachezaji kukabia juu kwa muda wote kwa sababu hawapo fiti. Aina hii ya mchezo inahitaji wachezaji wawe fiti na wamekula vyema huku wakisafiri katika mazingira mazuri.
Hawa akina Sadio Mane ambao wanakabia kuanzia juu wapo fiti. Wamekula vizuri. Wamelala vizuri. Mchezaji aliyesafiri kwa basi kutoka Kagera mpaka Mtwara akiwa amekunja miguu yake safari nzima, huku akiwa hajashiba vyema atapata wapi ubavu wa kukabia juu kwa dakika zote tisini?
Wachezaji wengi wanapenda kurudi na kuanza kukaba kuanzia chini kwa sababu wanajipumzisha. Wakiwa wanatembea wanarudi wanapata nafasi ya kupumzika.
Kuwaiga akina Pep na Klopp ni safari ndefu. Wakati tukiwa bado hatujafanya mambo mengi ya msingi, wao wanatuletea mengine mapya.