Juve kumtoa Dybala kumbeba staa Pogba

TURIN, ITALIA . JUVENTUS wanajipanga kuhakikisha wanatimiza ndoto zao za kumsajili kiungo wa Manchester United, Paul Pogba kwenye dirisha lijalo la usajili.

Kwenye mpango huo, miamba hiyo ya soka ya Italia imepanga ama kumtumia mshambuliaji Paulo Dybala au kiungo Miralem Pjanic kwenye dili la kuwashawishi Man United.

Pogba anaonekana kuwa kwenye nyakati zake za mwisho za maisha huko Old Trafford na huenda akaachana na timu hiyo kwenye dirisha lijalo la usajili huku Juventus wakimtaka mchezaji wao wa zamani arudi kwenye kikosi.

Real Madrid nao wanatajwa kuhitaji saini ya mchezaji huyo na hapo ndipo panapowafanya Juventus kutaka kuwapa Man United ofa ya mchezaji ili kushinda kwenye vita hiyo.

Man United wapo tayari kuachana na Pogba kama tu kutawekwa mezani Pauni 100 milioni huku mchezaji mwenyewe akidai kwamba atakasirika kama klabu hiyo itatumia kipengele kilichowekwa kwenye mkataba wake cha kuongeza mwaka mmoja zaidi wa kuendelea kubaki kwenye kikosi hicho. Mkataba wa sasa wa Pogba utafika tamati mwakani, lakini ndani yake kuna kipengele kinachowaruhusu Man United kumwongezea mwaka mmoja. Juventus wao wanamtaka na wapo tayari kuachana na mmoja wa wachezaji wao Pjanic na Dybala.