KMC: Uzoefu umeibeba TP Mazembe

Wednesday July 10 2019

 

By CHARITY JAMES

Dar es Salaam. Beki wa KMC, Abdallah Mfuko ameweka wazi sababu ya wao kufungwa na TP Mazembe ni kukosa uzoefu lakini pia, wenzao wamecheza pamoja kwa kipindi kirefu.
KMC ni wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kagame yanayoendelea nchini Rwanda,  jana Jumanne wameshindwa kupata matokeo dhidi ya Mazembe kwa kukubali kipigo cha bao 1-0.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mfuko alisema haukuwa mchezo rahisi kwao walipambana kuhakikisha wanapata matokeo lakini mbinu na uzoefu wa wapinzani wao ndio kitu kilichowanyima matokeo.
"Mazembe ni wazoefu wa mashindani sisi huu ndio msimu wetu wa kwanza, tuna kikosi kipya ambacho wachezaji wengi ndio kwanza wanaanza kujifunza mfumo mpya wa mwalimu kutokanana yule wa awali  kuondoka,"alisema Mfuko.
"Ukiachana na mimi ambaye nimejiunga na timu hii dirisha la usajili,  kuna wengine wameongezewa mikataba baada ya kukipiga kuanzia msimu uliopita wote tunaonekana ni wapya kwani ndio kwanza tumekutana na mwalimu mpya ambaye anapambana akutengeneza mfumo mpya."
Mfuko aliongeza, kufungwa kwao si mwisho wa mashindano bado wana nafasi ya kuendelea kupambana zaidi ili kjuweza kufikia mafanikio na kuongeza kuwa mashindano hayo watayatumia vyema kuhakikisha yanawapa uzoefu na kufahamiana.

Advertisement