Mhilu, kinara mabao Kagera afichua Zahera alivyozima ndoto yake Yanga SC

Mwinyi Zahera ametawala katika vinywa vya watu wengi kila mmoja akisema lake baada ya mkataba wake kusitishwa na klabu ya Yanga.

Zahera ameibua mjadala kwa wadau wapo wanaosema Yanga imefanya uamuzi sahihi na wengine wangependa kumuona kocha huyo akipewa muda hadi mkataba wake utakapomalizika msimu huu.

Jina la Zahera sasa ni maarufu zaidi kila kona vijana wa vijiweni wamtaja kwa mazuri na wengine wanatoa maoni tofauti wakimwelezea namna alivyotoa mchango wake ndani ya klabu hiyo.

Zahera aliingia kwa mguu mzuri Yanga, aliteka hisia za mashabiki wengi, wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kwa namna alivyoiongoza timu ikiwa inapitia kipindi kigumu cha ukata akichukua nafasi ya George Lwandamina.

Mbali na hao, lipo kundi jingine la wachezaji waliowahi kupita mikononi mwa Zahera nalo halikuwa nyuma kutoa maoni wakimchambua kwa mazuri na mabaya.

Yusuf Mhilu ni mmoja wa wachezaji waliopita mikononi mwa Zahera, lakini hakufaidi matunda ya kocha huyo raia wa DR Congo baada ya kudumu naye kwa muda mfupi.

Katika mazungumo na Spoti Mikiki, Mhilu anafichua namna kocha huyo alivyozima ndoto yake ya kucheza Yanga, klabu aliyokuwa akiipenda na kuitumikia kwa dhati.

Mhilu anasema Hans Van der Pluijm ndiye aliyemuibua kikosi cha pili baada ya kuvutiwa na kiwango chake na hata alipoondoka alimkabidhi kwa Lwandamina.

“Niliibuliwa na Hans baada ya kuridhishwa na kiwango alinipeleka timu ya kwanza, alipoondoka alikuja Lwandamina ambaye alinipa nafasi katika baadhi ya mechi ingawa sikucheza sana naye bahati mbaya aliondoka,”anasema Mhilu.

Anasema pamoja na makocha hao wa kigeni kutambua kipaji chake, hali ilikuwa tofauti kwa Zahera kwani hakuridhika naye, hivyo alimtoa kwa mkopo kwenda kuongeza kiwango.

“Zahera hakuridhishwa na kiwango changu akanishauri nitafute timu kwa mkopo ili kupandisha kiwango na baadaye nitarudi Yanga jambo ambalo niliona ni sahihi nikapata Ndanda,”anasema Mhilu.

Anasema baada ya miezi sita aliyodumu Ndanda alifunga mabao mawili na kusaidia mengine sita na kuiwezesha timu hiyo kumaliza msimu katika nafasi ya nane.

“Niliporudi Yanga baada ya msimu kumalizika kocha Zahera aliwaeleza viongozi anataka kubadili kikosi kwa kusajili wachezaji wapya, hivyo mimi sitaweza kupata namba,”anasema mchezaji huyo.

Anasema haikuwa rahisi kupokea uamuzi wa kocha kwa kuwa aliona ndoto yake imeanza kupotea, hivyo hakuwa na namna zaidi ya kuvunja mkataba uliokuwa wa miaka minne kwa makubaliano ya pande zote.

Winga huyo anasema alijiunga na Kagera Sugar na amekuwa chachu ya mafanikio ya klabu hiyo ambayo kabla ya mechi za mwishoni mwa wiki ilikuwa nafasi ya tatu.

Anasema siri ya kupata mafanikio Kagera yametokana na kucheza kwa nidhamu chini ya Kocha Mecky Maxime. Mhilu amefunga mabao manne katika Ligi Kuu.

“Ushindani ni mkali katika kikosi, lakini napambana kupata namba ya kudumu kwa kufuata maelekezo ya benchi la ufundi.

“Mimi si mshambuliaji ni winga kazi yangu ni kupandisha mashambulizi na wakati huohuo nasaidia kushambulia hatua inanifanya niwe mwepesi,”anasema Mhilu.

Mhilu anasema hajaridhika kufunga mabao manne na malengo yake ni kuhakikisha anachuana na Meddie Kagere wa Simba katika mbio za kutwaa tuzo ya mfungaji bora.

Mchezaji huyo mwenye ndoto ya kucheza Taifa Stars, anamtaja beki wa Simba Shomari Kapombe ni mlinzi hodari anayemvutia katika Ligi Kuu msimu huu.

“Timu iliyotupa wakati mgumu ni Alliance ingawa tulishinda mabao 2-1 lakini tulipata wakati mgumu,”anasema Mhilu ambaye ameziita mezani Simba na Yanga kama zinahitaji huduma yake katika usajili wa msimu ujao.

Mchezaji huyo aliitwa timu ya vijana cha Yanga mwaka 2016 akitokea Sifa United inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu Dar es Salaam kabla ya kutamba na Kagera Sugar.