Kagere, Bocco wamtesa Okwi

Muktasari:

  • Washambuliaji Meddie Kagere na John Bocco wamekuwa na kiwango bora msimu huu

Dar es Salaam. Pacha inayoanza kuzoeana ya nahodha John Bocco na Meddie Kagere inamuweka katika mazingira magumu Emmanuel Okwi kutetea zawadi ya ufungaji bora kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Tofauti na msimu uliopita ambao Okwi ndiye alikuwa mfungaji bora ndani ya kikosi cha Simba akicheza pacha na Bocco, safari hii mambo yameonekana kugeuka ambapo wachezaji hao wamekuwa wakianzishwa kama washambuliaji wa kati huku Okwi akipangwa kama mshambuliaji au winga wa pembeni.

Uamuzi wa kuwaanzisha Kagere na Bocco kama washambuliaji wa kati, umemfanya Okwi acheze mbali na lango tofauti na msimu uliopita ambao alipachika mabao 21 kwenye Ligi Kuu, akitumia vyema faida ya kucheza karibu na lango la timu pinzani.

Bocco ambaye ndiye alikuwa mpishi mkuu wa mabao ya Okwi, msimu huu amegeuka kuwa mpishi wa mabao ya Kagere hasa katika mechi za hivi karibuni kutokana na kile kinachoonekana kuanza kuzoeana katika staili ya uchezaji wao.

Tayari athari kwa Okwi imeanza kujionyesha kutokana na kupungua kwa kasi ya kufunga hadi sasa baada ya Simba kucheza mechi 16 kulinganisha na msimu uliopita.

Tofauti na msimu uliopita ambao hadi mechi ya 16 ya ligi, Okwi alikuwa amefunga mabao zaidi ya 15, hadi sasa mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda amefunga saba tu kwenye mashindano hayo.

Hata hivyo mabao hayo saba, Okwi amefunga katika mechi za mwanzoni mwa msimu huu ambapo Simba ilikuwa inatumia mfumo wa 4-3-3 ambao ulikuwa unamfanya asiwe mbali na lango tofauti na sasa ambapo timu hiyo inacheza 4-4-2.

Mfumo huo unamlazimisha Okwi kushuka chini kumsaidia beki wake wa pembeni lakini pia kutengeneza mashambulizi kutokea pembeni kwenda kwa Kagere na Bocco wanaocheza katikati.

Katika kudhihirisha hilo, tangu Simba ilipoanza kutumia mfumo wa 4-4-2, mabao ya Okwi kwenye Ligi Kuu yamekuwa yakikauka taratibu na rekodi zinaonyesha hajafunga katika mechi sita mfululizo za ligi ambazo Simba ilicheza dhidi ya Yanga, Mwadui FC, Singida United, KMC, Lipuli FC na JKT Tanzania.

Mara ya mwisho Okwi kufunga kwenye Ligi Kuu ilikuwa ni Oktoba 28 ambapo alipachika mabao matatu katika ushindi wa 5-0 dhidi ya Ruvu Shooting.

Kupungua kwa kasi ya kufunga mabao msimu huu kunatokana na ufanisi wa pacha ya Kagere na Bocco unajidhihirisha pia katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Okwi ambaye msimu uliopita alikuwa kinara wa Simba katika kufumania nyavu katika Kombe la Shirikisho waliloshiriki, hadi sasa amefunga mabao mawili tu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows ya eSwatini na JS Saoura ya Algeria.

Wakati Okwi akifunga mawili, Kagere ndiye tishio zaidi kwani amefunga mabao sita wakati Bocco amepachika wavuni mabao matatu.

“Nadhani Okwi bado ni mshambuliaji tishio na siamini kama kasi yake ya kufumania nyavu imepungua, bali sasa hivi anapangwa pembeni jambo linalomfanya asiwe karibu na lango lakini ni mchezaji ambaye anaweza akakuadhibu muda wowote pindi anapokaribia golini,” alisema kocha na mchambuzi Joseph Kanakamfumu.