Kagere, Okwi wakata utepe pazia kufuzu Afcon leo

Muktasari:

Mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Afcon 2021 yanashirikisha jumla ya timu 48 zilizogawanywa katika makundi 12 ambayo kila moja lina timu nne.

Dar es Salaam. Washambuliaji Meddie Kagere wa Rwanda na Emmanuel Okwi wa Uganda leo wataziongoza nchini zao katika michezo ya ufunguzi wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) Cameroon 2021.

Rwanda na Uganda ni miongoni mwa timu 16 zilizo katika makundi tofauti ya mashindano hayo ikiwa ni raundi yake ya kwanza.

Makundi matatu timu zake zitafungua dimba leo ni lile la B, F, I na L huku timu za makundi mengine zikipangwa katika siku zinazofuata kama ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) inavyobainisha.

Mshambuliaji wa Simba, Kagere ataiongoza Rwanda ugenini kuikabili Msumbuji kwenye Uwanja wa Zimpeto jijini Maputo, katika mchezo wa Kundi F.

Wakati Kagere akiwa Maputo nyota mwingine wa Simba, Okwi naye ataiongoza Uganda walio kundi B leo watakuwa ugenini huko Ouagadougou, Burkina Faso kukabiliana na wenyeji wao katika mchezo utakaochezwa Stade Du Aout na mechi nyingine ya kundi hilo leo itachezwa ndani ya uwanja wa Kamuzu Banda jijini Blantyre kuwakabili wenyeji Malawi.

Katika Uwanja wa Ahmadou Ahidjonc nchini Cameroon, wenyeji watakuwa wakiikaribisha Cape Verde ikiwa ni mechi ya kundi F.

Mechi nyingine za mashindano hayo ya kufuzu leo zitakuwa ni za kundi I ambapo katika Uwanja wa Septemba 24 jijini Bissau, wenyeji Guinea Bissau watawaalika Eswatini na katika uwanja wa Lat Dio, wenyeji Senegal watakuwa wakiikaribisha Congo.

Michezo ya L ndio itakayohitimisha mechi za kuwania kufuzu Afcon 2021 kwa siku ya leo ambapo Nigeria wataikaribisha Benin katika Uwanja wa Godswil Akpabio huko jijini Uyo na mechi nyingine itakutanisha wenyeji, Sierra Leone dhidi ya Lesotho ambayo itachezwa ndani ya dimba la Taifa jijini Freetown.