Kagere atamba eti Yanga nitawapiga mapema tu

KASI ya straika wa Simba, Mnyarwanda Meddie Kagere imeanza kuwatisha mabeki wa timu pinzani, lakini mwenyewe amefunguka akisema mbona bado sana.

Kagere ambaye msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, msimu huu ameanza kwa kishindo akifunga mabao mawili kwenye mechi ya ufunguzi dhidi ya JKT Tanzania katika ushindi wa mabao 3-1, amesema jukumu lake la kwanza ni kufunga na hatachagua timu ya kuifunga iwe watani zao wa jadi, Yanga na zingine zote ambazo zitakutana na Simba.

Alisema anapofunga anarahisha kutimia kwa malengo ya timu kushinda na kubeba mataji mbalimbali hivyo, hataacha kutekeleza jukumu hilo.

“Kazi yangu ni kufunga na ndio jukumu ambalo Simba wameniajiri kulifanya. Nitafunga kila nafasi ninayopata na bila kujali tunacheza na nani. Yanga haiwezi kunizuia kutelekeza kazi yangu uwanjani. “Tena tunapocheza na Yanga nakuwa na kiu ya kufanya vizuri zaidi ili kuwapa mashabiki furaha. Mabao niliyofunga msimu uliopita nataka kuongeza zaidi msimu huu na hilo litaifanya Simba kufikia malengo,” alisema Kagere ambaye msimu uliopita alifunga mabao 23 na kubeba kiatu cha dhahabu.

Alisema baada ya Simba kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wamehamishia nguvu Ligi Kuu Bara na wamekubaliana kujitoa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kila mechi.

“Natambua nina deni kubwa kutokana na kile ambacho nilikifanya msimu uliopita ili kuona nakirudia tena na hayo ndio malengo yangu na nimeanza safari ya kufikia huko,” alisema Kagere.

Msimu uliopita katika mechi ya pili Simba walicheza na Mbeya City na kushinda mabao 2-0, yote yali fungwa na Kagere ambaye mechi ya kwanza walicheza na Tanzania Prison walishinda 1-0, ambalo lilifungwa pia na msha mbuliaji huyo.

Kagere mpaka sasa kwenye kikosi hiko cha Simba ame weza kufunga mabao 44 katika mashindano yote tangu alipojiunga nayo msimu uliopita akitokea Gor Mahia ya Kenya.

Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems alisema alitegemea kumwona Kagere anavunja rekodi ya msimu uliopita kwa kuanza na mabao hayo dhidi ya JKT Tanzania.

Aussems alisema Kagere anacheza nafasi ya ushambuliaji hivyo, anatakiwa anapokuwa uwanjani kunusa harufu ya kufunga mabao kadri anavyopata nafasi.

“Nategemea kuona Kagere akifunga zaidi ya msimu uliopita kwani, uwezo anao na timu inacheza kwa kutengeneza nafasi nyingi, lakini umakini unakosekana na kama hili likibadilika si yeye tu bali hata washambuliaji wengine wanaweza kufanya hivyo,” alisema Aussems.