Kagere azusha hofu Simba, mwenyewe akimbilia kumtaja Niyonzima

Sunday September 9 2018

 

By CHARLES ABEL NA MWANAHIBA RICHARD

LICHA ya kuanza kwa kasi katika kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu Bara, straika wa Simba, Meddie Kagere ana shughuli pevu ya kuwafunika mastraika saba wa nguvu ambao wanaweza kumvurugia dili lake msimu huu.

Mbali na deni la kuhakikisha anaiongoza Simba kufanya vyema katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, ni wazi pia Kagere ana lengo la kuibuka mfungaji bora kwenye michuano hiyo na pia Ligi Kuu akiongoza kwa sasa akiwa na mabao matatu.

Hata hivyo, huku akianza kuonyesha uelekeo mzuri kwenye mbio za kuwania ufungaji bora wa Ligi Kuu msimu huu, Kagere amejikuta kwenye vita mpya dhidi ya washambuliaji saba ambao endapo hatojipanga vyema wanaweza kuwa kikwazo kwake na Simba kutikisa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Zikiwa zimebaki siku 81 kamili kabla ya Simba kuanza harakati zake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, tayari washambuliaji hao saba wameanza kutishia uwezekano wa Kagere na wenzake John Bocco na Emmanuel Okwi kutamba kwenye mashindano hayo yatakayoanza hatua ya awali kati ya Novemba 27 na 28.

Huku tayari jumla ya timu 42 zikiwa zimeshajihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kati ya 68 za jumla, kasi na kiwango bora cha washambuliaji hao saba kwenye mashindano hayo msimu huu na yale ya Kombe la Shirikisho kinaonekana ni moto wa kuotea mbali na iwapo Kagere, Okwi na Bocco wakishindwa kujipanga vyema hawatofua dafu mbele ya wakali hao.

Nyota hao saba ambao kama ilivyo kwa Simba, nao timu zao zimejihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ni Jean-Marc Makusu Mundele wa AS Vita Club, anayeshika nafasi ya pili kwenye Kombe la Shirikisho akiwa na mabao saba.

Mastaa sita waliopo kwenye chati ya ufungaji bora kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambao tayari timu zao zimejihakikishia kushiriki mashindano hayo msimu ujao ni pamoja na Bean Malango (TP Mazembe), Walid Azaro (Al Ahyl), Anice Badri (Esperance), Felix Badenhost (Mbabane Swallows), Hamid Addad (Wydad Casablanca) na Ocansey Mandela (Horoya).

Malango ndiye kinara wa ufungaji kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika hadi sasa akiwa na mabao saba akifuatiwa na Azaro mwenye mabao sita sawa na Badri.

Addad wa Wydad Casablanca ana mabao matano wakati Badenhost wa Mbabane Swallows na Mandela wa Horoya wenyewe wana mabao manne kila mmoja.

Tayari, TP Mazembe iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pamoja na washindi wao wa pili, AS Vita wamejihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kama ilivyo kwa Esperance nchini Tunisia.

Wydad Casablanca nayo imejihakikishia kuiwakilisha Morocco baada ya kumaliza nafasi ya pili kwenye ligi yao wakati Al Ahly yenyewe imejikatia tiketi yake mapema baada ya kutwaa ubingwa wa Misri.

Horoya na Mbabane Swallows zenyewe zimefanikiwa kutwaa ubingwa kwenye Ligi Kuu katika nchi zao ambazo ni Guinea na Swaziland hivyo jambo linalozipa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Advertisement