Kakolanya arejeshwa Taifa Stars

Muktasari:

  • Katika kikosi hiko, Ettiene amemrejesha kipa Beno Kakolanya anayeichezea Simba hivi sasa, ambaye awali alikuwa katika kikosi hiko kabla ya kuwa katika matatizo na kikosi cha Yanga.

MECHI tatu ambazo Beno Kakolanya amezicheza akiwa na Simba katika mechi za kimataifa, zimemrejesha kipa huyo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinachojiandaa kuivaa Burundi katika mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2022.
Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Etienne Ndayiragije jioni hii ametangaza kikosi cha wachezaji 30 akimjumuisha, Kakolanya ambaye alienguliwa enzi za Kocha Emmanuel Amunike kufuatia kushindwa kuitumikia Yanga waliokuwa na mzozo nao wa kimasilahi.
Kakolanya aliachana na Yanga na kuhamia Simba na kuumia kwa kipa mwenzake, Aishi Manula kulimpa nafasi ya kucheza mechi dhidi ya Power Dynamos ya Zambia katika Tamasha la Simba Day kisha kuisaidia Simba kutoka suluhu ugenini kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrioka dhidi ya UD Songo na baadaye Azam katika Ngao ya Jamii.
Nafasi yake ndani ya Stars ilichukuliwa na kipa wa sasa wa Yanga Metacha Mnata na kurejea kwake kumemfanya Aaron Kalambo wa Mbeya City kuchomolewa kikosini, huku kiungo Ally Ng'anzi anayeichezea Minessota ya Marekani naye ameitwa katika kikosi hicho kwa mara ya kwanza, licha ya awali kuichezea timu ya taifa ya Vijana U17.
Wengine waliojumuishwa kwenye kikosi hicho kipya cha Stars ni Eliuter Mpepo wa Buildcorn ya Zambia na Mohammed Issa 'Banka' (Yanga) na kikosi kamili cha Kocha Ndayiragije  anayeinoa Azam FC kwa sasa ni makipa; Beno Kakolanya, Juma Kaseja na Metacha Mnata.
Mabeki ni; Shomari Kapombe, Hassan Kessy, Gadiel Michael, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Boniface Maganga, Kelvin Yondani, Idd Mobby, Erasto Nyoni na Abdi Banda,  huku viungo wakiwa ni; Jonas Mkude, Baraka Majogoro, Himid Mao, Ally Ng'anzi, Abubakar Salum, Frank Domayo, Abdulazizi Makame, Hassan Dilunga na Mohammed Banka.
Washambuliaji ni; Simon Msuva, Eliuter Mpepo, Mbwana Samatta, Adi Yusuph, Farid Mussa, Idd Seleman 'Nado', Kelvin John, Ayoub Lyanga na Shaaban Idd Chilunda.