Kamusoko aweka ugumu Yanga

YANGA itakuwa na kibarua kigumu ugenini kuifunga Zesco kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuruhusu sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kuelewana kwa viungo wa Yanga, dakika 45 za kipindi cha kwanza, kuliisaidia timu hiyo kumiliki mpira na kuwapa urahisi washambuliaji kufika langoni mwa wapinzani wao mara kwa mara.
Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera aliwachezesha Abdullaziz Makame, Feisal Salum 'Fei Toto', Mohamed Issa 'Mo Banka' na Papy Tshishimbi waliokuwa wanamuelewano mzuri wa kuichezesha timu.
Banka na Fei Toto walifanya kazi vyema ya kupeleka mashambulizi mbele ambapo dakika ya 22 Yanga ilipata bao kwa mkwaju wa penalti iliochongwa na Patrick Sibomana.
Penalti ya Yanga ilitokana na makosa ya beki wa Zesco ambaye alimkwaa Sydney Urkho na Sibomana akaipiga kwa ustadi.
Makame naye hakuwa nyuma kusaidiana na mabeki kukaba ambapo aliwapa tabu viungo wa Zesco waliokuwa wanaongozwa na mchezaji wao wa zamani Thaban Kamusoko.
Zesco haikukata tamaa baada ya kuwa nyuma kwa bao 1-0 na kama si uimara wa ukuta wa Yanga, dakika 45 za kipindi cha kwanza huenda wangesawazisha bao kwani walikuwa wanafika mara kwa mara langoni kwa wapinzani wao.
Ukuta wa Yanga uliongozwa na Kelvin Yondan, Lamine Moro, Ally Mtoni 'Sonso' na Mapinduzi Balama licha ya kucheza kiungo katika mechi hiyo alichezeshwa namba mbili.
Licha ya Mapinduzi kutokuwa mzoefu na michuano ya kimataifa alionekana kumdhibiti kiungo wa Zesco United, Jesse Were na bado yao ilionekana kuwa kivutia kwa namna ambavyo walikuwa wanachuana.
Kitendo cha Zahera kufanya mabadiliko kipindi cha pili, alimtoa Mo Banka na kumuingiza Mrisho Ngassa safu ya kiungo ilionekana kupunguza uimara wake na uelewano wa mabeki ulianza kuwa mdogo baada ya kuingia Ali Ali aliyechukua nafasi ya Mapinduzi aliyekuwa ameumia.
Yanga ilijikuta inaandamwa na washambuliaji wa Zesco ambao muda mwingi walikuwa ndani ya 18 ya mlinda mlango Mnata.
Zesco ilisubiri dakika za majeruhi kusawazisha bao kupitia kwa Thaban Kamusoko ambaye ni mchezaji wa zamani wa Yanga.
Mabadiliko ya Yanga, kocha Zahera alimtoa Banka/ Ngassa, Maybin Kalengo/Sydney huku Mapinduzi aliumia nafasi yake ilichukuliwa na Ali Ali.

KAULI YA MAKAME
Sare ya bao 1-1 ilimuumiza kiungo wa Yanga, Abdulaziz Makame alisema kwamba matokeo hayo yamemuumiza na yanakuwa yanawapa wakati mgumu kwenye mechi ya marudiano.
"Hatuwezi kukata tamaa lakini itakuwa mechi ngumu kwani tayari Zesco itakuwa na bao la ugenini, ingawa hatujakata tamaa tunaamini tutakwenda kupambana ili tuweze kusonga mbele"alisema.

KAMUSOKO AKOSA RAHA
Pamoja na Kamusoko kuisawazishia timu yake ya Zesco dakika za majeruhi alisema inashindwa kuizungumzia Yanga kwa sababu aliichezea zamani.
"Nashindwa kusema chochote kuhusiana na Yanga kwa sababu nimekaa nayo kwa amani, sikuwa na budi kupambana kwa ajili ya kuisaidia timu yangu ya Zesco kushinda," alisema.