Kaseja aachwa Kilimanjaro Stars

Dar es Salaam. Kipa Juma Kaseja amejumuika katika orodha ya wachezaji tisa walioachwa katika safari ya kwenda Uganda kwenye mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya kuwania Kombe la Chalenji kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo kuwa majeruhi na kuugua.

Kilimanjaro Stars iliondoka jana jioni kuelekea Uganda tayari kwa mashindano hayo huku kocha mkuu wa kikosi hicho, Juma Mgunda akitamba kufanya vizuri lakini kubwa lililowastua wengi ni kuachwa kwa kipa namba moja Juma Kaseja kutokana na majeraha ya goti.

Kaseja ambaye amekuwa mhimili tangu aliporejeshwa tena katika kikosi cha Taifa Stars Julai mwaka huu ameidakia timu hiyo michezo tisa ya mashindano ikiwamo miwili dhidi ya Kenya, Burundi na Sudan na mmoja dhidi ya Guinea ya Ikweta na Libya na mmoja wa kirafiki dhidi ya Burundi.

Wachezaji wengine mabao wameachwa katika kikosi hicho kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya ni Salum Kimenya anayeumwa malaria, Iddi Seleman’ Nado’, Salum Abubakary ‘Sure Boy’, Shaaban Idd Chilunda na Frank Domayo walio majeruhi pamoja na Kelvin John, Yusuph Mhilu, Abdulmajid Mangalo na Fred Tangalu.

Wachezaji walioondoka ni makipa Aishi Manula, Metacha Mnata na David Kisu, mabeki Juma Abdul, Nickson Kibabage, Gadiel Michael, Mwaita Gereza, Mohamed Hussein, Kelvin Yondani na Bakari Mwamnyeto wakati viungo ni Baraka Majogoro, Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Hassan Dilunga, Zawadi Mauya, Cleoface Mkandala na washambuliaji Ditram Nchimbi, Miraji Athuman, Eliuter Mpepo, Lukasi Kikoti na Rashid Chombo