Kashfa ya ukwepaji kodi yamtesa Messi

Muktasari:

Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi amesema alitaka kuondoka Hispania baada ya kukumbwa na kashfa ya ukwepaji kodi mwaka 2017

Madrid, Hispania. Lionel Messi ametamka kwa mara ya kwanza alitaka kuondoka Barcelona kutokana na sakata la ukwepaji kodi.

Nahodha huyo wa Barcelona alisema kitendo cha kudaiwa na Serikali amekwepa kodi ya Pauni2.95 milioni kilimuweka njiapanda.

Messi alipigwa faini ya Pauni 223,000 kwa kosa hilo ambalo alisema lilitaka kuharibu maisha yake Nou Camp mwaka 2017.

Hata hivyo, alisema anashukuru kashfa hiyo ya ukwepaji kodi kati ya mwaka 2007 na 2009 ilimpata wakati watoto wake wakiwa na umri mdogo.

“Nilitaka kuondoka si Barcelona, nilitaka kuihama Hispania. Nilidhani sikutendewa haki na sikutaka kuendelea kuishi hapa,”alisema Messi.

Mshambuliaji huyo alisema alikuwa na wakati mgum yeye na familia yake kwa kuwa kashfa hiyo ilikuwa kubwa kwake.

Tangu alipojiunga na Barcelona Novemba 2003, amefunga mabao 604 katika mechi 692 alizocheza Barcelona.