Kasi ya Kenya yamtisha kocha Ngorongoro Heroes

Muktasari:

  • Ngorongoro Heroes itachuana na Kenya kesho Jumanne saa 7:00 mchana ukiwa muendelezo wa mshindano ya Cecafa Chalenji yanayofanyika nchini Uganda.

Dar es Salaam. Kiwango kilichoonyeshwa na Kenya cha kuifunga Zanzibar mabao 5-0, kimemshtua kocha wa timu ya Taifa ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 20,'Ngorongoro Heroes', Zubery Katwila amekiri vijana wake wanatakiwa kujituma zaidi watakapoikabili timu hiyo kesho Jumanne.

Ngorongoro Heroes itachuana na Kenya kesho Jumanne saa 7:00 mchana ukiwa muendelezo wa mshindano ya Cecafa Chalenji yanayofanyika nchini Uganda.

Huo unakuwa mchezo wa pili kwa Ngorongoro Heroes baada ya mchezo wa kwanza uliofanyika jana Jumapili kuifunga Ethiopia kwa mabao 4-0.

Timu hiyo itaikabili Kenya iliyoichapa Zanzibar mabao 5-0.

Katwila alikuwepo uwanjani kuwafuatilia wapinzani wake alisema kwa namna alivyoitazama Kenya vijana wake wanatakiwa kucheza kwa kujituma zaidi ili kupata ushindi wa pili na kutinga hatua ya robo fainali ya mashindani hayo.

“Tumewaona Kenya, ni timu nzuri. Niliwaangalia mechi na Zanzibar. Uzuri ni kwamba hata wachezaji wangu pia walikuwepo uwanjani na kuona wapinzani wetu wamefanya kitu gani.

"Mchezo baina yetu utakuwa mzuri, mgumu na wenye ushindani, lakini natumaini tutafanya vizuri," alisema Katwila.

Naye beki wa kati wa timu hiyo, Oscar Masai alisema wachezaji wote hawana hofu na Kenya watakayopambana nao kwani tayari kocha wao amewapa mbinu za kuwakabili.

"Wachezaji tuko tayari kwa mchezo huo kwani ushindi wa mechi ya kwanza umetuongezea morali. Kuhusu Kenya, kocha aliwaona na ametuambia nini cha kufanya hapo kesho,”alisema Masai.