Kazi imeanza ... majeruhi wafumua benchi Yanga

Thursday October 17 2019

 

MABOSI wa Yanga wameshtukia jambo moja ambalo lilianza kama utani, kabla ya kubaini limewapotezea mastaa wao wa maana na sasa kuna akili moja waliyopanga kufanya ili kulifumua benchi lao la ufundi lililopo chini ya Kocha Mwinyi Zahera.

Wiki mbili kabla ya mchezo wao wa mtoano (playoff) wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya misri, Yanga imekuwa na changamoto kubwa juu ya kuibuka kwa idadi kubwa ya majeruhi ambapo kabla ya wiki hii kulikuwa na nyota 12 waliotengeneza chumba cha majeruhi ikiwa ni sawa na kikosi kizima.

Hata hivyo, mpaka sasa kuna unafuu fulani, baada ya ya wachezaji wengi waliokuwa majeruhi kuanza kurejea na uongozi wao ukasema kuna mabadiliko wanaweza kuyafanya kuwanusuru na tatizo hilo wanaloliona limekuwa sugu katika timu yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo aliliambia Mwanaspoti kuwa hali iliyopo sasa ya idadi kubwa ya majeruhi hasa wakielekea kukutana na Pyramids inawanyima raha na wanafikiria kukifanyia tathmini kitengo chao cha matibabu na kama vipi huenda wakafanya mabadiliko makubwa.

“Tuna taarifa na hilo la idadi ya majeruhi, hali haipo vizuri na tunapambana kama uongozi kuhakikisha mambo yanakuwa sawa kwa kutafuta matibabu ya haraka ya hawa wachezaji wote walio majeruhi,” alisema Gumbo.

“Hali siyo nzuri kweli, lakini tunashukuru sasa wapo ambao wameanza kurejea taratibu baada ya kupata matibabu, lakini sambamba na hilo uongozi wetu unalifanyia tathmini benchi la ufundi hasa kitengo cha matibabu.”

Advertisement

Aliongeza kuwa, “kuna madaktari bingwa tuko nao katika mazungumzo ambao ni Yanga wenzetu na wengine ndio hawa wanaowatibu sasa vijana wetu walioanza kurejea, hili litaenda mbali zaidi kwa kuangalia hata kuwaajiri madaktari wengine, hapo tutaangalia daktari tuliye naye sasa kama anatosha katika eneo hili au kipi tukifanye.

“Tukiona hatoshi tutaangalia cha kufanya na kama tutaona anatosha au aongezewe nguvu nalo tutaliangalia, lakini sasa itoshe kusema kwamba tupo katika mchakato mkubwa wa kuboresha eneo hili.”

Kwa sasa, Yanga ipo chini ya Dk Edward Bavu, ambaye jana alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi juu ya hali ya majeruhi wasiopona Jangwani akiwamo kiungo Juma Mahadhi, aliahidi angepiga mwenyewe, kitu ambacho hata hivyo hakukifanya na hata alipotafutwa tena alisisitiza atapiga na aachwe afanye mambo yake.

ISHU YA NGOMA

Aidha, Gumbo alisema kuondoka kwa straika wao wa zamani Donald Ngoma aliyepo Azam FC akiwa majeruhi, kisha baadaye kuanza kucheza pia kunachangia mabadiliko hayo huku pia wakifanya mchakato wa kuwakatia bima ya afya wachezaji wao.

Ngoma aliyekuwa staa muhimu Yanga alisitishiwa mkataba Jangwani Mei 19 kisha Mei 26 akatua Azam FC akiwa majeruhi na kupelekwa kwa matibabu nchini Afrika Kusini na kisha kurejea kuitumikia timu hiyo mpaka sasa.

“Unaweza kuangalia kesi kama ya Ngoma, hapa kwetu tulimvunjia mkataba kutokana na rekodi yake ya majeruhi, lakini baadaye akaenda timu nyingine kule wakamtibia akarudi kucheza na anaendelea kucheza,” alisema.

“Utaona hapo akili ya harakaharaka itakwambia hapa kwetu kuna kitu hakipo sawa katika mfumo wa matibabu yetu, uongozi wetu utalipatia ufumbuzi hili lakini pia tupo katika mchakato wa kuwakatia bima ya afya wachezaji wetu.”

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Dismas Ten alipotafutwa kutoa ufafanuzi juu ya kuwepo kwa mabadiliko hayo ya benchi la ufundi upande wa daktari, alisema hakuwa na taarifa ila akataka pewe muda afuatilie kisha angetoa taarifa.

BIGIRIMANA, KASEKE FRESHI

Katika hatua nyingine nyota wengine wawili wa Yanga waliokuwa majeruhi Issa Bigirimana na Deus Kaseke wamerejea uwanjani wakiungana na waliorejea juzi kwenye mchezo wa kirafiki wa Yanga dhidi ya Friends Rangers akiwamo Mrisho Ngassa, Sadney Urikhob, Papy Tshishimbi, Patrick Sibomana, Paul Godfrey ‘Boxer’ na Lamine Moro,

Wachezaji hao wameanza kupiga tizi na wenzao na kazi sasa kubaki kwa Kelvin Yondani, Ally Mtoni ‘Sonso’, Juma Mahadhi, Mohammed Issa ‘Banka’ na Cleofas Sospeter ambao hali zao inaelezwa bado, huku Yanga ikikabiliwa na mechi mbili ngumu jijini Mwanza - moja ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao FC na nyingine dhidi ya Waarabu wa Pyramids - zote zikitarajiwa kuchezwa Uwanja wa CCM Kirumba.

Advertisement