Kichuya achekelea kutua Bungeni

Wednesday May 16 2018

 

By Olipa Assa, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya, amesema timu hiyo imestahili kwenda bungeni kutokana na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa staili ya kipekee ikilinganishwa na Watani wao wa Jadi, Yanga ambao walichukua ubingwa msimu uliopita kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.

Kichuya, ambaye amechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya Simba msimu huu akifunga mabao saba na kutoa pasi 20 za mabao, alisema kitendo cha timu yake kupata mwaliko Bungeni kinatoa ishara kwamba Wabunge wamethamini na kuheshimu mafanikio ya klabu hiyo msimu huu ikilinganishwa na timu nyingine.

“Nadhani suala la kwenda Bungeni si ushamba bali inaonyesha ni kwa jinsi gani klabu yetu imepewa heshima kubwa na Bunge Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwani tumetwaa ubingwa tukiwa mbele ya wapinzani wetu kwa tofauti kubwa ya pointi lakini pia tumewazidi kwa tofauti kubwa ya mabao ya kufunga.

Wanaoikejeli Simba kwa kwenda Bungeni nadhani wanafanya kosa kubwa kwa sababu wanamaanisha kwamba viongozi waliotupa mwaliko walikosea jambo ambalo halina mashiko,” alitamba Kichuya.

Katika hatua nyingine, mchezaji wa zamani na kocha wa Simba, Abdallah Kibaden ameitaka timu hiyo kutobweteka na ubingwa waliouchukua na badala yake watumie kipindi hiki kujiandaa na ushiriki wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

“Ninachoweza kuwashauri waanze maandalizi mapema ya Klabu Bingwa Afrika, ili kuepuka kuishia hatua za awali, waje wafanye kitu cha tofauti kuonyesha kimya chao kilikuwa na kishindo,” alisema Kibaden.

Advertisement