Kichuya apewa mchongo Simba

Muktasari:

Shiza Kichuya tangu arejee upya Msimbazi, amecheza mechi chache kwa muda usiofikia hata dakika 60 kutokana na kukosa nafasi ya kuaminiwa mbele ya Kocha Sven Vanderbroeck.

NYOTA wa zamani wa Mtibwa Sugar, Abdallah Juma 'AJ' amemuangalia winga wa Simba, Shiza Kichuya kisha anampa neno akimtaka akubali kuanza moja ili aweze kurejea kwenye ufalme wake.
Mkonge huyo anayeshikilia nafasi ya pili ya kuwa straika aliyewahi kufunga mabao mengi ndani ya msimu mmoja nyuma ya Mohammed Hussein 'Mmachinga', amesema kwa kuwa, umri bado unamruhusu Kichuya kufika mbali na kucheza timu yoyote hapa nchini na nje ya nchi kwa sharti la kutambua alipojikwaa na kuanza upya kwani ndivyo soka lilivyo.
Amesema vazi la ustaa kwa sasa anatakiwa kuliweka pembeni na kutetea kiwango chake ili kurudisha thamani yake.
"Anachotakiwa kukifanya Kichuya kwa sasa nikujituma kwa bidii na mazoezi pia iwe funzo kwake kujua sifa alizokuwa anapata ni kwa sababu ya kazi yake na sio yeye," amesema Juma aliyefunga mabao 25 katika msimu wa 2004, moja pungufu aliyefunga Mmachinga mwaka 1999.
Ameongeza wachezaji wengi wanakwama kutokana na kulewa sifa nakusahau kupambania vipaji vyao.
"Tanzania ina vipaji vya juu tatizo ni wachezaji wanashindwa kuona mamilio yaliopo mbele wanalewa na vipesa vidogo,"
"Wanshindwa kuiga mfano wa staa wa kizazi chao Mbwana Samatta namna anavyopambana mpaka anapata heshima kubwa, sijui wanakwama wapi," amesema.