Kikosi cha Taifa stars kutangazwa muda wowote, Nani na nani wataitwa?

Muktasari:

  • Fainali za Chan zitafanyika kuanzia Aprili 4 hadi 25 mwaka huu huko Cameroon ambapo zitashirikisha timu za taifa kutoka mataifa 16 ambazo zimegawanywa katika makundi manne yenye timu nne kila moja.

BAADHI ya timu zitakazoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) zimeanza kutangaza vikosi vyao vya awali ikiwa ni mwanzo wa maandalizi kwa mashindano hayo yatakayofanyika huko Cameroon kuanzia Aprili 4 hadi 25 mwaka huu.
Timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ni miongoni mwa washiriki wa mashindano hayo ikiwa imepangwa kundi D sambamba na Zambia, Namibia na Guinea, ikishiriki kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2019.
Hivi karibuni kocha mkuu wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije naye atatangaza kikosi chake cha awali kinachotarajiwa kuwa na takribani wachezaji 32 kwa ajili ya maandalizi ya mashindano hayo ambayo bingwa wake anapata kitita cha Dola 1.25 milioni (Sh 2.8 bilioni)
Viwango bora vya wachezaji katika mashindano ya ndani bila shaka ndivyo vitachangia kuvutia benchi la ufundi kuwaita lakini kwa wale ambao wameshindwa kuonyesha ufanisi katika klabu zao wana uwezekano finyu wa kuwemo katika kikosi cha awali na hata kile kitakachoenda Chan ambacho kitatangazwa na benchi la ufundi la Stars.
Ingawa uamuzi wa mwisho juu ya nani awemo na nani asiwemo kikosini unabakia kwa kocha Ndayiragije na benchi lake la ufundi, makala hii inajaribvu kutabiri majina ya wachezaji wanaoweza kuwemo katika kikosi cha awali cha Stars kutokana na jinsi walivyoonyesha kiwango bora katika ligi lakini pia sababu nyingine zinaweza kuchagiza kama vile uzoefu na nidhamu binafsi ya mchezaji husika.
Makipa
Hapana shaka kupona kwamajeraha ya ya goti ya Juma Kaseja kumepunguza presha kwa benchi la ufundi la Stars kwani kipa huyo ndiye amekuwa chaguo la kwanza la Ndayiragije kutokana na kiwango bora ambacho amekuwa akikionyesha lakini anabebwa na uzoefu na uwezo mkubwa wa kusoma mchezo na kuipanga timu.
Tayari ameanza mazoezi mepesi pia wapo makipa wanaofanya vizuri kwa sasa waliokaa mkao wa kula ambao ni Aishi Manula wa Simba, Metacha Mnata (Yanga), Soud Dondola (Coastal Union), Mohamed Makaka (Ruvu Shooting), Benedictor Tinoco (Kagera Sugar), Mohamed Yusuph (Polisi Tanzania) na Ally Mustafa (Ndanda0
Wenye nafasi kubwa ya kuitwa ni Kaseja, Metacha, Manula na Dondola ingawa hao wengine wanaweza kupata fursa hiyo.
Mabeki wa pembeni
Imezoeleka upande wa kushoto mara kwa mara huwa wanaitwa Mohamed Hussein 'Tshabalala' na Gadiel Michael ambao wote wanachezea Simba lakini kwa kipindi hiki kuna uwezekano finyu kwa Gadiel kujumuishwa kwani hapati nafasi katika klabu yake na wapo wachezaji ambao wanafanya vizuri kwenye timu zao wanaocheza nafasi hiyo hiyo kama vile Yassin Mustafa (Polisi Tanzania), Ally Ramadhan (KMC), Issa Rashid (Mtibwa) na David Luhende (Kagera Sugar)
Tshabalala na Mustafa wana uwezekano mkubwa wa kuitwa kikosini
Upande wa beki wa kulia wenye nafasi ya kuitwa ni Juma Abdul (Yanga), Shomary Kapombe (Simba), Kibwana Shomary (Mtibwa) na Miza Christom (Namungo FC)
Mabeki wa kati
Nyakati zinaonekana kuwatupa mkono mabeki Erasto Nyoni na Kelvin Yondani na bila shaka kwa sasa ni uzoefu wao tu ndio unaweza kuwapa nafasi kikosini lakini wapo vijana azaidi yao ambao bila shaka wanahitajika kuanza kuingizwa taratibu kikosini ili wawe tegemeo la muda mrefu kutokana na ubora wanaoonyesha katika ligi.
Yondani, Nyoni na Aggrey Morris uhakika wa kuitwa kwao ni 50% kwa kila mmoja lakini yupo kijana Bakari Mwamnyeto ambaye tangu alipoitwa katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Rwanda mwaka jana amekuwa na mwendelezo mzuri wa kiwango.
Lakini wapo mabeki wanaofanya vizuri kama Abdallah Mfuko (KMC), Iddy Mobb (Polisi Tanzania), Dickson Job (Mtibwa), Juma Nyoso (Kagera Sugar), Ibrahim Ame (Coastal) na Abdulmajid Mangalo (Biashara United)
Wanaoweza kuitwa ni Morris, Yondani, Nyoni, Job, Mangalo, Ame, Mwamnyeto na Mobby
Viungo
Kuna vita kubwa nafasi ya kiungo na hapa bila shaka benchi la ufundi litaumiza sana kichwa.
Kwa viungo wa ulinzi wapo Jonas Mkude (Simba), Pato Ngonyani na Baraka Majogoro (Polisi Tanzania), Novatus Dismas (Biashara), Zawadi Mauya (Kagera Sugar), Mudathir Yahya (Azam FC), Abdulhalim Humud (Mtibwa Sugar), Jumanne Elfadhili (Prisons) na Mzamiru Yassin (Simba)
Upande wa viungo washambuliaji kuna Lucas Kikoti (Namungo), Salum Abubakar (Azam), Mapinduzi Balama (Yanga), Hassan Dilunga (Simba), Salum Kimenya (Prisons) na Juma Nyangi (Alliance FC)
Majina ambayo yana nafasi kubwa ya kuitwa ni Mkude,Dilunga, Mzamiru, Majogoro, Mauya, Mudathir, Kikoti, Balama, Kimenya na Abubakar
Washambuliaji
Kundi kubwa la washambuliaji wazawa limekuwa halifanyi vyema msimu huu ingawa wachache wamejitahidi kuchomoza na kuonyesha kiwango bora, wengi wao wanaonekana kukosa uzoefu wa kuweza kuhimili vishindo vya mashindano magumu kama Chan.
Wale wenye uzoefu wengi hawafanyi vizuri jambo ambalo ni wazi kwamba litapasua vichwa vya mabosi wa benchi la ufundi la Taifa Stars katika uteuzi.
Namba zinambeba Reliants Lusajo kwani ndiye mzawa aliyefunga idadi kubwa ya mabao Ligi Kuu hadi sasa akiwa nayo mabao 10 lakini nyuma yake wapo Yusuf Mhilu wa Kagera Sugar mwenye mabao tisa,  Daruwesh Saliboko na Paul Nonga wa Lipuli wenye mabao nane ingawa kuna Kelvin Sabato (Kagera Sugar), Sixtus Sabilo (Polisi), Vitalis Mayanga (Ndanda ) wanaofanya vizuri.
Wapo ambao hawafungi mabao lakini kigezo cha uzoefu kinaweza kutumika nao ni Shaban Chilunda, Ditram Nchimbi na John Bocco (Simba), Issah Abushehe (Coastal)
Utabiri wa kikosi kiujumla
Kutokana na tathmini hiyo ya juu, utabiri wa kikosi cha awali kitakachoitwa na benchi la ufundi la Stars kinaweza kuwa hivi
Makipa
Kaseja (KMC), Manula (Simba), Metacha  (Yanga), Dondola (Coastal)
Mabeki
Nyoni, Tshablala na Shomary Kapombe (Simba), Yondani, Abdul (Yanga), Morris (Azam), Mwamnyeto na Ame (Coastal Union), Mobby na Mustafa (Polisi Tanzania), Mangalo (Biashara) na Job (Mtibwa)
Viungo
Kikoti (Namungo), Mauya (Kagera Sugar), Abubakar na Yahya (Azam), Balama (Yanga), Majogoro (Polisi), Dilunga, Mkude na Mzamiru (Simba),
Washambuliaji
Bocco (Simba), Nchimbi (Yanga), Nonga (Lipuli), Abusheh (Coastal), Sabilo (Polisi), Chilunda (Azam) na Lusajo (Namungo)